Raia 104 wa Ethiopia watiwa mbaroni baada ya kupatikana wakiishi kwenye nyumba ya vyumba vitatu Juja

Na LAWRENCE ONGARO

RAIA 104 wa Ethiopia walinaswa eneo la Juja katika Kaunti ya Kiambu.

Inadaiwa walipatikana katika mtaa wa Matangi, Juja wakiishi katika nyumba yenye vyumba vitatu.

Kamanda wa polisi eneo la Juja Bi Dorothy Migarusha alisema raia hao wa kigeni walinaswa Jumatatu alfajiri wakiwa wamerundikana kwenye nyumba hiyo na wengi wao walishindwa kuwasiliana kwa lugha ya Kiingereza.

Waliokamatwa wana umri wa kati ya miaka 15 hadi 40.

Afisa huyo alieleza kuwa wakazi wa eneo hilo waliwashuku wageni hao ambao kwa muda wa wiki mbili wamekuwa wamejifungia mle ndani bila kuonekana nje.

“Maafisa wa polisi walifika eneo hilo na kuwapata wakiwa wamejifungia hadi walipolazimishwa kufungua,” alieleza afisa huyo.

Inadaiwa watu wawili pia walikuwa ndani ya nyumba hiyo ikionyesha kuwa wao ndio walikuwa wapishi.

Washukiwa hao walifungiwa katika kituo cha polisi cha Juja huku wakitarajia kusafirishwa Nairobi ili kuhojiwa zaidi katika kitengo cha Transnational Crime kabla ya hatua ya kisheria kuchukuliwa dhidi yao.

“Tunashuku kuna watu fulani wanaoendesha ulanguzi wa watu ili kuwasafirisha kwingineko. Kwa hivyo wakihojiwa zaidi tutajua ukweli wa mambo,” alifafanua afisa huyo.

Baada ya kufanya upekuzi, maafisa wa usalama walipata vyeti vya usafiri – pasipoti – viwili pekee.

Alieleza maafisa wa usalama wanaendelea kusaka mmiliki wa nyumba walimokuwa wakiishi wageni hao.

Wananchi wamepongezwa kwa kuonyesha uzalendo na kupiga ripoti kwa polisi kwa kushuku raia hao wa kigeni.