Polo ajuta kutafuna kuku na mayai yake

Na NICHOLAS CHERUIYOT

NAROK Mjini

BAROBARO mmoja wa mji huu alifinywa na kisha kutimuliwa na shugamami wake kwa kunyemelea binti yake.

Duru zasema kuwa, polo alianza uhusiano wa kimapenzi na mama huyo mwaka uliopita na wakaendelea vizuri licha ya pingamizi kutoka kwa familia ya polo.

Kulingana na mdokezi, jamaa alishauriwa aepukane na shugamami naye akashikilia kuwa anachuma mali akijitayarisha kuoa katika siku za usoni.

“Siwezi kuoa nikiwa sina mali. Nitamlisha binti wa wenyewe na nini? Nikiwahi donge kutoka kwa shugamami, nitaanzisha biashara na kumtema,” barobaro akasema akipinga wazo la kutengana na shugamami.

Juzi mambo yalienda kombo binti ya shugamami alipofika nyumbani kutoka chuo kikuu baada ya kupata likizo na mate yakamdondoka polo.

“Mama ya binti alipoondoka nyumbani kufanya shughuli zake, barobaro alimrushia demu mistari lakini kipusa akafura na kumfokea kwa tetesi za kumkosea heshima,” mdaku akaeleza.

“Unadhani mimi ni demu wa kawaida? Mimi siwezi kukubali mlofa kama wewe awe mpenzi wangu. Hata tayari nimejipanga kwa kumpata mpenzi anayesoma chuoni kama mimi. Nitakuripoti kwa mama,” kipusa alifoka.

“Eti utaniripoti? Maajabu! Mimi ndiye nitapendekeza uchukuliwe hatua kali na mama kwa kukosa heshima. Hata usijaribu kuyasema haya, mamako ataona unapayuka tu ovyo,” jamaa akasema kwa majigambo kisha akatoka kuelekea kwao.

“Siku iliyofuata, jamaa alifika kwa boma la mama sukari lakini mwenyeji wake akampa makaribisho baridi. Alipoona hali si hali, jamaa alijaribu kutoroka lakini shugamami huyo wa miraba minne akamtia mkononi na kumfinya sana kisha kumpiga teke kwa kugeuka fisi mtafuna vifaranga,” mdaku akaeleza.