• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Korti yaonyeshwa video ya mwili wa Sharon, kesi dhidi ya Obado ikianza

Korti yaonyeshwa video ya mwili wa Sharon, kesi dhidi ya Obado ikianza

Na RICHARD MUNGUTI

KESI ya mauaji dhidi ya Gavana wa Migori Okoth Obado na watu wengine wawili ilianza kusikilizwa Jumatatu, huku mahakama ikionyeshwa picha na video za kutisha za mwili wa Sharon Otieno na mwanawe aliyetarajia kumzaa.

Kimya kilitanda kortini Jaji Cecilia Githua na waliohudhuria walipotazama kwa mshtuko picha hizo za miili ya Sharon na mwanawe aliyekuwa na wiki 28 tumboni.

Mpasuaji Mkuu wa Maiti Dkt Johansen Oduor alisema, vifo vilitokea baada ya Sharon na mwanawe kuvuja damu nyingi.

Upasuaji ulionyesha Sharon alikuwa na majeraha saba makubwa yaliyosababishwa na kifaa chenye makali. Kifaa hicho pia kilimjeruhi mtoto aliyekuwa tumboni na kuchomozea mgongoni mwake.

Video iliyonyesha Dkt Oduor akipasua maiti hizo mbili na hatimaye akichukua sampuli za kufanyiwa uchunguzi wa DNA.

Mpasuaji huyo wa Serikali alikuwa shahidi wa kwanza katika kesi hiyo ambapo Obado ameshtakiwa pamoja na Casper Obiero (aliyekuwa msaidizi wa Obado) na mfanyakazi wa kaunti ya Migori Michael Oyamo.

Ilidaiwa mauaji hayo yalitekelezwa Septemba 3, 2018 katika eneo la Owade kaunti ndogo ya Rachuonyo, Homa Bay.

Sharon alikuwa na umri wa miaka 26 alipouawa.

Wakili Kioko Kilukumi anayemwakilisha Obado akiwa na Bw Rodgers Sagana aliuliza Dkt Oduor ikiwa mmoja anaweza kuuawa kabla ya kuzaliwa.

Akijibu Dkt Oduor alisema, “Mimi si wakili. Siwezi kueleza ikiwa mtoto ambaye hajazaliwa anaweza kuuawa au la. Hilo ni suala la kupambanua kisheria.”

Mawakili wengine waliomhoji Dkt Oduor ni Prof Tom Ojienda na Elisha Ongoya.

Obado, Obiero na Oyamo waliachiliwa kwa dhamana walipokana mashtaka dhidi yao.

“Sababu ya kuchukua sampuli za DNA na kujaribu kuwatambua waliowaua Sharon na mwanawe,” Dkt Oduor alisema.

Kesi imeendelea leo Jumanne.

You can share this post!

Radi yaua 60 wakiwemo 11 waliokuwa wakipiga ‘selfie’

Omar Hassan kupata ushindani mkali katika kuwania tiketi ya...