• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
TAHARIRI: Serikali ikae ange kuzima utekaji

TAHARIRI: Serikali ikae ange kuzima utekaji

KITENGO CHA UHARIRI

HIVI majuzi Wizara ya Usalama ilitangaza mikakati yake ya kukabiliana na changamoto za kiusalama nchini kuanzia mwezi huu hadi wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Miongoni mwa mikakati hiyo ni kukabiliana na utovu wa usalama katika kipindi cha kampeni na siasa za 2022, pamoja na kikosi maalum cha kupambana na utekaji nyara.

Japo, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i alipuuzilia mbali kina cha visa vya utekaji nyara Kenya, ni hatua ya kufurahisha kuwa aliunda kikosi hicho.

Hata ingawa Waziri Matiang’i alitilia shaka kukithiri zaidi kwa visa hivyo, ripoti za vyombo vya habari na mitandao zinapozingatiwa, hakika visa vya watu kupotea vimekuwa vingi zaidi nchini katika siku za hivi majuzi kuliko wakati mwingine wowote.

Maadamu shule zinafungwa wakati wowote kuanzia leo hadi Ijumaa ya kesho kutwa, ni muhimu vikosi vya usalama vikae ange kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayeathirika.

Vikosi vya usalama vihakikishe vimetoa njia na mikakati ya kuripoti mara moja tukio lolote la utekaji mbali na kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa wahalifu hao wamekamatwa.

Kwa sababu ya matarajio hayo ya kuongezeka kwa uovu huo ambao umekuwa tatizo sugu, sharti kila mmoja awe makini zaidi kutibua matukio ya aina hiyo.

Waama, hili ni jukumu la kila Mkenya wala halipaswi kuachiwa vyombo vya usalama pekee. Naam, vikosi vya usalama vina jukumu kubwa la kutekeleza maadamu ndivyo vilivyopewa jukumu kubwa na la kimsingi la kudumisha usalama.

Hata hivyo, kila Mkenya, hasa wazazi wanaombwa kuwapa watoto wao tahadhari dhidi ya wahalifu hao waliojaa nchini kwa sasa.

Watoto wakatazwe kuchukua zawadi zozote kutoka kwa watu wasiowajua pamoja na kukataa usaidizi wowote kutoka kwa watu wa sampuli hiyo.

Serikali itakuwa imesaidia pakubwa iwapo itatoa mwongozo unaoweza kuwasaidia wazazi na walezi kuwapa watoto wao mafunzo ya kukabiliana na tatizo hilo sugu.

Aidha, ni muhimu jinsi Wizara ya Usalama ilivyosema kuwa, taifa linapoelekea katika uchaguzi mkuu, pana uwezekano mkubwa wa visa hivi vya utovu wa usalama kuzidi, na hivyo basi kuwepo haja ya kubuni mikakati madhubuti ya kuvizuia mapema.

You can share this post!

BURUDANI: Matamanio ya Dizo Cappy ni kunguruma ndani ya WCB...

Mashabiki wataka kocha Mikel Arteta apigwe kalamu baada ya...