• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
GWIJI WA WIKI: Neema Salome Sulubu

GWIJI WA WIKI: Neema Salome Sulubu

Na CHRIS ADUNGO

UIGIZAJI ni kazi kama kazi yoyote nyingine.

Kufaulu katika ulingo huo wa sanaa kunahitaji jitihada, stahamala na nidhamu ya hali ya juu.

Usijitose katika uigizaji kwa lengo la kutafuta fedha na umaarufu. Hutadumu ulingoni kwa muda mrefu!

Hatua ya kwanza katika safari ya mafanikio ni kufahamu unachokitaka, kujielewa wewe ni nani, kutambua unakokwenda na kupiga hatua kusonga mbele kuelekea huko unakolenga kufika.

Mtangulize Mungu katika kila hatua unayoipiga. Kipende unachokifanya na namna unavyokifanya. Yafanye mambo yaliyomo ndani ya uwezo wako. Yafanye kwa utaratibu unaofaa na kwa wakati unaostahili. Fanya hivyo ili ufike mbali!

Kuwa mwepesi wa kusikiliza na mpole zaidi katika kunena. Hakuna ajifunzalo mtu asiyeuliza. Uliza wajuao ili nawe ujue!

Huu ndio ushauri wa Bi Neema Salome Sulubu – mwanahabari mbobevu na mwigizaji stadi wa vipindi vya runingani.

MAISHA YA AWALI

Neema alizaliwa katika mtaa wa Kisumu Ndogo, eneo la Malindi, Kaunti ya Kilifi. Amekulia katika familia ya Waadventista wa Sabato (SDA).

Ndiye wa saba kuzaliwa katika familia ya watoto wanane wa Bi Janet Dama na marehemu Bw Sulubu Mwagandi Ngala. Nduguze Neema ni Mary Mapenzi, John Kiponda, Lilian Sikukuu, Mercy Rehema, Ashley Asha, Esther Kaneno na marehemu Samson Safari.

Safari yake ya elimu ilianzia katika chekechea ya Al-Fauz, Malindi. Alijiunga baadaye na Shule ya Msingi ya HGM Malindi kisha Shule ya Upili ya Ngala Memorial, eneo la Watamu, Kilifi (2006-2009).

Baada ya kusomea uanahabari katika Chuo cha Mombasa Aviation kati ya 2011 na 2013, Neema alijiunga na chuo cha Kenya Institute of Management (Bewa la Mombasa) mnamo 2017 kusomea masuala ya usimamizi na mahusiano ya umma. Alihitimu katika mwaka wa 2019.

UIGIZAJI

Uigizaji ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Neema akiwa na umri mdogo. Marehemu mwalimu Maulidi alikuwa mwepesi wa kumjumuisha katika makundi ya kutumbuiza wageni kwa nyimbo na mashairi nyakati za hafla mbalimbali shuleni Al-Fauz.

Baadaye katika shule ya msingi, walimu walitia azma ya kupalilia kipaji walichokitambua ndani ya mwanafunzi wao huyu. Bi Munyao alimpa Neema majukwaa mengi ya kuwa ngoi (kiongozi stadi wa nyimbo) katika mashindano ya viwango tofauti.

Alitamba kwa wepesi kutokana na umilisi wake wa Kiswahili.

Uwezo wa Neema katika ulumbi uliwahi kumfanya maarufu sana miongoni mwa wanafunzi wenzake katika shule ya msingi baada ya kuongoza wimbo ‘Katililo’ kwa ukakamavu wa kuajabiwa.

Wengine waliomwamshia ari ya kuthamini na kuchapukia masuala ya uigizaji ni Bw Joseph Akwiri, Bw Kadenge, Bi Maitha na Bw Muye Marembo ambao walitangamana naye kwa karibu sana katika shule ya upili.

Kipaji kinachojivuniwa na Neema katika ulingo wa uigizaji kilipaliliwa zaidi na kutiwa nakshi na Bw Elphas Shitandi na Bw Mbashir Shambi ambao pia walimpokeza malezi bora ya kiakademia katika Chuo cha Mombasa Aviation.

VIPINDI NA TUZO

Neema aliwahi kuongoza makundi mbalimbali ya wanafunzi kutoka Shule ya Msingi ya Malindi, Shule ya Upili ya Ngala Memorial na Chuo cha Mombasa Aviation kushiriki tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Alijizolea tuzo ya Mwigizaji Bora katika michezo ya jukwaani (2008, 2009, 2013) na akatwaa taji la haiba kubwa la ‘Adjudicators’ Award’ mnamo 2007 kwenye tamasha za kitaifa zilizoandaliwa Tumutumu Girls, Kaunti ya Nyeri.

Mnamo 2012, alijiunga na kundi la waigizaji katika Shirika Lisilo la Kiserikali la S.A.F.E Kenya Pwani. Aliwaongoza wenzake kuhamasisha umma kuhusu masuala ya afya, ugaidi pamoja na umuhimu wa kudumisha amani na kuhifadhi mazingira.

Mchezo wa kwanza wa runingani ambao Neema alishiriki ni ‘Utandu’. Aliigiza mhusika Nana katika mchezo huo uliotolewa na Ashiner Pictures mnamo 2013.

Baada ya milango ya heri kujifungua, alipata fursa ya kuigiza mhusika Tumu katika ‘Moyo’ (2014-2016). Huo ndio mchezo uliomkweza kwenye ngazi ya juu zaidi katika ulingo wa uigizaji.

Mnamo Disemba 2018, Neema alitawazwa Mwigizaji Bora wa Kenya Coast Music Awards.

Aliwahi pia kuigiza mhusika Binti katika mchezo ‘Aziza’ (2016-2019) kabla ya kuanza kuigiza Neema katika mchezo ‘Zora’ ambao hufyatuliwa na Citizen TV kila Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa moja unusu hadi saa mbili usiku.

UANAHABARI

Neema aliajiriwa na redio ya Baraka 95.5 FM mnamo Julai 2013 kuwa prodyusa wa kipindi ‘Bumburuka’ kilichokuwa kikiperushwa hewani kila wikendi.

Umahiri wake wa kuzamia masuala ya kiuchumi ulimfanya pia kuaminiwa fursa ya kuwa mwendeshaji wa kipindi ‘Kurunzi ya Biashara’.

Upekee wake wa kuoanisha talanta na kozi alizozisomea ulimpigisha hatua kubwa katika juhudi za kuwekea taaluma ya uanahabari uhai.

Hadi alipoondoka Baraka FM mnamo Disemba 2018, Neema alikuwa mkuu wa Kitengo cha Matangazo na majukumu yake yalikuwa kuandaa ripoti muhimu na kuratibu matangazo ya biashara.

JIVUNO

Anapojitahidi kujiimarisha zaidi katika sanaa, Neema yuko mstari wa mbele kuwapokeza vijana wenzake kunga za kujinoa vilivyo na kujikuza katika ulingo wa uigizaji.

Hutumia ujuzi wa kuigiza kuwaelekeza waumini wenzake katika Kanisa la Malindi Central SDA kuhusu masuala ya maadili na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali maishani.

Anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo sasa inatawala chipukizi wengi ambao wametangamana naye katika majukwaa mbalimbali ya uigizaji.

Neema anawastahi sana wamiliki wa kampuni ya Jiffy Pictures – Lulu Khadija Hassan na Rashid Abdalla – kwa kumpa fursa ya kudhihirisha utajiri wa kipaji chake cha uigizaji kupitia michezo ‘Moyo’, ‘Aziza’ na ‘Zora’.

You can share this post!

Polisi wakanusha kujua aliko mwanamume aliyetoweka Lamu...

KINA CHA FIKIRA: Wazazi watie bidii kuwalinda watoto wao...