• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Mbegu zilizotolewa kwa Sharon si za Obado, washukiwa

Mbegu zilizotolewa kwa Sharon si za Obado, washukiwa

Na RICHARD MUNGUTI

SAMPULI za shahawa zilizotolewa kwa mwili wa Sharon Otieno siku aliyouawa hazikuwa za Gavana wa Migori Okoth Obado wala washtakiwa wawili wenza Michael Oyamo na Casper Obiero, mahakama kuu ilielezwa Jumatano.

Lakini mtaalamu wa maabara ya serikali aliyefanya uchunguzi wa chembe-jeni (DNA) alisema Bw Obado ndiye baba wa mtoto wa Sharon Otieno aliyeuawa kabla ya kuzaliwa.

Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Cecilia Githua, mtalaam huyo, Bw John Kimani Mungai aliyefanya ukaguzi wa DNA kwenye shahawa zilizotolewa katika uke wa Sharon, alisema hazikuwa za watatu hao.

Bw Mungai alieleza Jaji Githua, kuwa sampuli za shahawa zilizotolewa kwa uke wa Sharon hazikulingana na sampuli kutoka kwa Bw Obado, Oyamo na Obiero.

Alisema uchunguzi wa DNA ulionyesha shahawa alizopewa zilikuwa za watu tofauti na wala hazikulingana na za Oyamo na Obiero.

Bw Mungai anayesimamia maabara ya Serikali, alimweleza Jaji Githua, “Shahawa zilizotolewa kwa uke wa Sharon zilikuwa za watu waliombaka Sharon na hatimaye kumuua. Hazikuwahusu wawili hao.”

Shahidi huyo ambaye amehudumu katika maabara ya serikali kwa siku 30, alisema Oyamo na Obiero wanaowakilishwa katika kesi hiyo na Prof Tom Ojienda na Prof Elisha Ongoya mtawalia, hawakuhusika.

“Je, ulipopima sampuli za shahawa ulizopewa na Polisi ulikuwa unajaribu kuwabaini waliotekeleza mauaji ya Sharon,” Prof Ojienda alimuuliza Bw Mungai.

“Ndiyo,” Bw Mungai alijibu.

“Lakini je, uchunguzi huo wa DNA unawaondolea Oyamo na Obiero lawama kuwa walikuwa sehemu alikouawa Sharon,” Prof Ojienda aliuliza shahidi huyo.

Bw Mungai alisema sampuli alizopokea kutoka kwa afisa wa uchunguzi Bw Nichola ole Sena kutoka kwa mwili wa Sharon hazikuwa za Mabw Oyamo na Obiero.

Mahakama ilielezwa Bw Obado ndiye baba halisi wa mtoto wa Sharon kulingana na ukaguzi wa sampuli za DNA zilizotolewa kwa Obado na kijusi hicho kilichokuwa na uri wa wiki 28.

Kutokana na ukaguzi wa vipimo vya DNA ilibainika Bw Obado ndiye baba ya mtoto huyo kwa asilimia 99.9.

“Oyamo sio baba ya mtoto huyo wa Sharon,” alisema Bw Mungai.

Bw Mungai alisema vifaa vingine alivyopewa kupima vilikuwa na damu iliyokuwa ya binadamu.

Vifaa hivyo ni sidiria, mfuto na viatu vilivyopatikana eneo alikouawa Sharon katika msitu wa Kondea, Kaunti ya Homa Bay.

You can share this post!

Kesi ya Jumwa kuanza mwaka 2022

TAHARIRI: Tamko kumhusu Raila halikustahili