• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:25 PM
TAHARIRI: Tamko kumhusu Raila halikustahili

TAHARIRI: Tamko kumhusu Raila halikustahili

KITENGO CHA UHARIRI

MSIMU wa kampeni za Uchaguzi Mkuu ujao umeanza kuingia, zaidi ya mwaka mmoja mapema.

Ingawa kulingana na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kampeni rasmi zafaa kuanza Aprili mwaka ujao, wanasiasa wameanza kuuza sera zao kwa wapigakura.

Katika harakati za kuvutia uungwaji mkono, wanasiasa wameanza kutumia propaganda, uongo na hata semi za chuki.

Matamshi ya baadhi yao wiki hii, yanaashiria kwamba kunahitajika juhudi na hatua kali kuchukuliwa. Wanasiasa wameanza kutoa cheche za maneno yanayoweza kuichoma nchi, sawa na ilivyoshuhudiwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Baadhi ya viongozi kutoka eneo la Ukambani walisikika wakiwachochea wakazi kwamba safari nyingine Rais Uhuru Kenyatta akitembelea eneo lao, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga asiandamane naye.

Kauli hiyo ni ya kutisha ambayo ingawa huenda ilitolewa kwa nia njema, inaweza kutumiwa kuzua uhasama wa kikabila nchini.

Bw Odinga ni mshirika wa Rais Kenyatta kwenye mapatano ya handisheki. Kwa yeye kuandamana na Rais Ukambani, bila shaka alialikwa na Rais. Shughuli za Rais hufanywa kwa mpangilio maalum na katu haiwezekani kwa mtu yeyote kushtukizia au kuingia ‘kwa mlango wa nyuma’.

Hata kama kweli Bw Odinga hakualikwa, ni Rais Kenyatta aliyepaswa kulalama, si viongozi wa chama cha Wiper.

Kudai kwamba walitaka kuzungumza na Rais Kenyatta masuala ya Ukambani pekee na Bw Odinga hakupaswa kuwa huko, ni makosa.

Kwanza, Katiba inaruhusu kila Mkenya kutembea popote nchini, isipokuwa maeneo yaliyotengwa kiusalama kama vile ikulu.

Isitoshe, kinara wa Wiper Stephen Kalonzo Musyoka ni kiongozi wa kitaifa kama Bw Odinga. Atatarajiwa kutembea nchi nzima kunadi sera zake atakapowania urais mwaka 2022.

Je, itakuwaje iwapo watu wa ngome ya Bw Odinga nao wataamua kuwa Bw Musyoka naye asikanyage huko? Siasa za chuki, uhasama na kuwataja watu wengine vibaya zimepitwa na wakati.

Wananchi wanapaswa kuwauliza wanasiasa maswali magumu kuhusu sera zao, si kuwaunga mkono eti kwa sababu wanamchukia mtu wanayetaka waamini ni adui yao.

Tume ya Uwiano na Utangamano (NCIC) yapaswa kuonyesha makucha yake, kwa kuwazuia watu wa aina hii kuzua fujo nchini.

You can share this post!

Mbegu zilizotolewa kwa Sharon si za Obado, washukiwa

KINYUA BIN KING’ORI: Wanaopinga Zuma kufungwa...