• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
KINYUA BIN KING’ORI: Wanaopinga Zuma kufungwa wanastahili adhabu kali

KINYUA BIN KING’ORI: Wanaopinga Zuma kufungwa wanastahili adhabu kali

Na KINYUA BIN KING’ORI

HATUA ya wafuasi wa aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kuanzisha maandamano yanayolenga kuzua machafuko nchini humo kulalamikia kufungwa kwa rais huyo wa zamani aliyegonga umri wa miaka 79 ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miezi 15 gerezani, inafaa kulaaniwa vikali, wala haifai kuigwa na mataifa mengine.

Rais huyo wa zamani alihukumiwa kifungo hicho na mahakama ya kikatiba kwa kukaidi amri iliyomtaka atoe ushahidi kuhusu kesi ya ufujaji mali ya umma alipokuwa mamlakani.

Wafuasi wa kiongozi huyo mwenye kashfa nyingi wanadai uamuzi huo wa mahakama ni maonevu na ubaguzi wala haukufikiwa kwa haki. Inasikitisha kutambua wakati mataifa mengi ulimwenguni yanasifia mahakama ya Afrika Kusini kwa kutoa mfano mwema wa jinsi mahakama za mataifa mengine yakiwemo ya bara la Afrika hasa ukanda wa Afrika Mashariki, zinavyofaa kujitolea kuwakabili wafisadi.

Viongozi wengi wa mataifa hayo huishi kutumia fedha za umma kwa ubadhirifu mkubwa na kukaidi amri za korti bila kujali sheria maana wao hujiona kwamba wako juu ya sheria kwa kupofushwa na mamlaka. Mataifa mengi duniani yameishia uchumi kuporomoka na maisha ya wananchi kuathirika vibaya, kutokana na hulka ya viongozi walio uongozini kutumia kila mbinu kufaulisha njama za ufisadi kwa kuiba fedha za umma.

Ikiwa mahakama za Kenya zinataka kusaidia nchi hii kumaliza ufisadi na kuinua maendeleo yetu zianze kuiga umahiri ulioonyeshwa na mahakama ya kikatiba ya Afrika Kusini kwa kuwafunga viongozi ambao wamekuwa mashujaa wa kupuuza maagizo ya korti hata wengine wakikosa kushirikiana na korti kutoa ushahidi juu ya kesi zinazowahusu na kuishia kutupwa kwa ukosefu wa ushahidi.

Korti zinaweza kuchangia kuimarisha maendeleo na kuokoa fedha za umma zinazoporwa na viongozi walafi hasa wanasiasa wenye tamaa na uroho. Mfano huo mpya wa Afrika Kusini unaweza kusaidia na kutia ari vita dhidi ya janga la ufisadi ikiwa utakumbatiwa na mahakama zetu na idara zingine zilizotwikwa jukumu la kupambana na wafisadi na hata kukomesha kabisa mtindo wa viongozi wanaoshikilia nyadhifa kuu serikalini kudharau maagizo ya korti kwa kukaidi amri zao bila hofu.

Lakini hilo kufaulu, ni raia kuelewa wanastahili kushirikiana na idara za mahakama maana wamepewa uwezo na katiba kuhakikisha viongozi wote wanawaongoza kwa mujibu wa katiba.

Hivyo wanafaa kuhakikisha viongozi kuanzia kwa Rais Uhuru Kenyatta hadi kwa mwakilishi wadi hawaepuki mkono wa sheria ikiwa atathibitishwa ni mhusika katika kashfa za ufisadi au kupuuza amri za mahakama.

Hebu niulizie, wakazi wa eneo la Kwa Zulu-Natal wanaotatiza amani na utulivu nchini mwao kwa kuandamana kuharibu mali ya umma wakitaka Zuma aachiiliwe huru, wanajua madhara ya ufisadi?

Je, wanaelewa mshukiwa wa ufisadi ndiye aliyejifaidi mwenyewe binafsi na fedha zao ambazo zingaliwafaa kuimarisha maisha yao vijijini?.

Kwa vile ufisadi ndio kizuizi katika safari ya kujenga taifa bora, lenye usalama thabiti, litakuwa jambo la busara raia kukoma kutetea mafisadi wakishtakiwa na kufungwa, badala yake wawe mbele kushirikiana na mahakama na serikali kuangamiza janga la ufisadi ambalo limeishi kutishia uchumi na maendeleo ya mataifa mengi, Kenya ikiwemo.

Inaudhi kwamba raia nchini Kenya pia hawana tofauti na wakazi wa Zulu-Natal, kiongozi wao akishtakiwa tu na kuhusishwa na ufisadi wacha kufungwa gerezani kama Jacob Zuma, watajitokeza mchana wa jua la utosi kulalamikia hatua ya kiongozi wao kuonewa na kuhusishwa na visa vya ufisadi.

Hata viongozi wengine wamekuwa wakitumia makabila au mirengo kisiasa yao kama kisingizio cha kuonewa wakilenga tu kupotosha umma.

Kwa Sababu wananchi nao wamekuwa wakiamini upotovu huo imekuwa vigumu vitendo vya ufisadi kukomeshwa.

Lakini, ikiwa mahakama zitaendelea kuwahukumu bila kuzingatia hisia Za Jamii, Serikali pamoja na wananchi waunge mkono ufisadi Utakuwa kitendawili nchini kuanzia serikali za kaunti hadi ya kitaifa. Utakuwa ushindi mkubwa kwetu sote kama taifa.

La mno, ni viongozi kusaidia mataifa yao kufanikiwa kiuchumi, kisiasa na kiustawi Kwa kuangamiza ufisadi Kwa kujitenga na maovu hayo.

Kupambana na ufisadi na viongozi waovu wasiozingatia Sheria si jukumu la mahakama pekee bali Jamii ambayo inafaa kuwakemea maana kuwashangilia ni kuwafanya mashujaa na itakuwa kibali wao waendelee kutumia mamlaka yao kuendeleza ufisadi Kwa kunajisi uchumi na maendeleo ya nchi Kwa kufuja pesa na Mali ya umma

You can share this post!

TAHARIRI: Tamko kumhusu Raila halikustahili

KAMAU: Waraka wa wazi kwa wenyeji wa Kiambaa