• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:55 AM
KAMAU: Waraka wa wazi kwa wenyeji wa Kiambaa

KAMAU: Waraka wa wazi kwa wenyeji wa Kiambaa

Na WANDERI KAMAU

HII ni barua ya wazi kwa wenyeji wa eneobunge la Kiambaa.

Hamjambo? Leo ni siku muhimu sana kwenu mnapofanya maamuzi kuhusu yule atakayekuwa mbunge wenu kwa karibu mwaka mmoja ujao.

Kwa takriban mwezi mmoja uliopita, tumeshuhudia kampeni zenye ushindani mkali baina ya mirengo mikuu ya kisiasa nchini, kila mmoja ukilenga kudhihirisha ubabe wake.

Mirengo hiyo pia imekuwa ikikosoana kwa kuelekezeana kila aina ya lawama.

Ushindani mkuu umekuwa ukionekana kati ya vyama vya Jubilee na UDA, kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto.

Kimsingi, uchaguzi huu unafasiriwa kuwa ushindani wa kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto, kwenye matayarisho ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Hata hivyo, mnapofanya maamuzi yenu, lazima mfahamu kuwa kiongozi mtakayemchagua atachangia pakubwa katika kutoa mwelekeo wa maisha yenu kisiasa na kiuchumi.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto hawatakuwepo, ikiwa mtamchagua kiongozi ambaye baadaye atawasahau na kupotelea jijini Nairobi.

Ni lazima mfahamu kuwa vigogo hao wawili ni wanasiasa ambao lengo kuu ni kuendeleza maslahi na ushawishi wao kisiasa.

Rais Kenyatta analenga kuimarisha usemi wake kuhusu mchakato wa kumrithi. Naye Dkt Ruto analenga kutathmini mpenyo wake kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya.

Waswahili walisema kuwa; ‘Fahali wawili wapiganapo, nyasi ndizo huumia’.

Kwa muda wa miaka mitatu iliyopita, siasa za Kenya zimefunikwa na mvutano wa kisiasa kati ya Rais Kenyatta na naibu wake, baada ya Rais kubuni handisheki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Baada ya muafaka wa vyama vya TNA na URP mnamo 2012, wawili hao waliwaahidi Wakenya “mapambazuko mapya” ya kisiasa nchini.

Hili lilifuatia ghasia zilizotokea nchini baada ya uchaguzi tata wa 2007/2008, ambapo zaidi ya Wakenya 1,300 walipoteza maisha yao.

Licha ya ahadi hiyo, wawili hao wameivunja. Wamesahau namna ambavyo Wakenya walisimama nao, hasa walipokabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kibinadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), mjini Hague, Uholanzi.

Hili linatufunza kuwa kama wananchi, ni makosa kuwaamini wanasiasa na ahadi wanazotoa kwetu.

Je, ni nani angeamini kuwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto wangekosana? Ni nani angeamini kuwa kauli ya ‘UhuRuto’ ingevunjika na kuwafanya wafuasi wao kugawanyika katika makundi mawili hasimu? Ni nani angedhani kuwa ukanda wa Mlima Kenya ungegeuka kuwa jukwa la makabiliano makali ya kisiasa kati ya wawili hao?

Vivyo hivyo, hakuna yeyote angeamini ikiwa Rais Kenyatta angebuni usuhuba wa kisiasa na Bw Odinga, hasa baada yao kurushiana cheche kali za maneno kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2017.

Funzo kuu tunalopaswa kupata kutokana na mwelekeo huo ni kuwa wanasiasa huwa hawatujali hata kidogo.

Lengo lao huwa ni kuwafarakanisha wananchi kwa maslahi na manufaa yao wenyewe. Huwa wanawatumia watoto wa wananchi wa kiwango cha chini kushiriki maandamano na harakati zingine za kudhihirisha ‘ubabe’ wao.

Mnapomchagua mbunge mpya, nawaomba mzingatie sifa na utendakazi wake wala si mrengo wa kisiasa anaoegemea.

Hilo ndilo litakalowahakikishia uwepo wa kiongozi anayejali maslahi yenu.

Ahsanteni na kila la kheri.

[email protected]

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Wanaopinga Zuma kufungwa...

Eliud Kipchoge alenga kufanya kitu atakachokumbukwa nacho...