• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
MATHEKA: Serikali inawatesa raia kwa kuongeza ushuru kiholela

MATHEKA: Serikali inawatesa raia kwa kuongeza ushuru kiholela

Na BENSON MATHEKA

KWA wakati huu ambao Wakenya wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha, kuna uwezekano raia wengi watapata msongo wa mawazo kutokana na hatua ambazo serikali inachukua.

Ingawa serikali imekuwa ikitangaza na kupigia debe hatua inazodai ni za kupunguzia raia mzigo wa gharama ya maisha, hali ni tofauti kabisa na hatua inazodai inachukua kusaidia mwananchi wa kawaida ni mchezo wa uhusiano mwema tu.

Ukweli wa mambo ni kuwa hakuna uwezekano wa gharama ya maisha kupungua nchini Kenya kwa kuwa hakuna hatua thabiti ambayo imechukuliwa au inayopangwa kuchukuliwa na serikali, kwa nia njema, kusaidia mwananchi wa kawaida.

Hii ni kwa sababu inachofanya serikali ni kuongeza ushuru wa bidhaa muhimu bila kutoa huduma kwa walipa-ushuru.

Kwa hakika, inachofanya serikali ni kuhadaa, kutesa na kuadhibu umma kwa kuongeza ushuru wa bidhaa muhimu.

Inachokosa kueleza umma, na ambacho si siri, ni kwamba pesa inazokusanya zinalipa madeni. Kwa wakati huu, na hii si siri pia, serikali inategemea Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) kufadhili bajeti yake huku ikitegemea Benki ya Dunia kufadhili miradi.

Ni kuadhibu raia kuendelea kuongeza karo ya shule wakati ambao ushuru unaendelea kuongezeka.

Ni kuhadaa Wakenya kwamba kuna afya kwa wote kisha wanapofika katika hospitali za umma wanatumwa kununua dawa kwenye maduka ya kibinafsi wakati ambao wanalala njaa na kukosa kodi ya nyumba ilhali wanatozwa ushuru wa juu unaopaswa kutumiwa kuimarisha huduma za afya.

Ni kutesa Wakenya serikali inapoweka mazingira yanayowafanya kutopata mikopo ya kupanua biashara zao.

Ni kuwaongezea mateso raia kwa kuanzisha mtaala mpya wa elimu unaowaongezea mzigo wakati wengi wao hawana ajira kutokana na mazingira mabaya ya kiuchumi.

Ni hali hii ambayo imewasababishia Wakenya wengi kukumbwa na msongo wa mawazo na ongezeko la ukosefu wa usalama nchini.

Matokeo yake ni watu kujiua na kuua wengine, watu kuibiwa mali hata mchana na dhuluma za nyumbani kuongezeka.

Gharama ya kukabiliana na hali hii ni kubwa kuliko kuweka na kutekeleza sera zinazokuza uchumi wa Mkenya wa kawaida.

Bila hali ya uchumi kubadilika, hali hii itadumu kwa muda nchini na athari zake zitakuwa mbaya na ghali mno.

Huu ndio ukweli ambao waliosababisha hali hii hawataki kusikia na badala yake wanatumia uongo kuuficha.

Sikitiko zaidi ni kwamba waliosabisha hali hii hawataona haya kurudi kwa raia kutumia masaibu wanayopitia kuwaomba kura katika uchaguzi mkuu ujao. Naam, huu ndio ukweli; wanasiasa watatumia umaskini wanaosababishia raia kuomba kura kwa kuwaahidi mbingu huku wakiwahonga kwa pesa wanazopora kwa kutengea mradi hewa.

Kutesa wananchi kwa kuongeza ushuru ni njia moja ya kuwafanya wasiweze kujikuza kiuchumi, kuongeza karo ni kufanya maskini asisomeshe watoto waweze kufunguka macho na kutetea haki zao. Huu ndio ukweli na hali ya kusikitisha nchini.

You can share this post!

PSG wamsajili kipa Gianluigi Donnarumma wa Italia bila ada...

WASONGA: Ruwaza za kiuchumi zao Ruto, Raila ni hadaa tupu