• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
WASONGA: Ruwaza za kiuchumi zao Ruto, Raila ni hadaa tupu

WASONGA: Ruwaza za kiuchumi zao Ruto, Raila ni hadaa tupu

Na CHARLES WASONGA

MIONGOZO ya kiuchumi ambayo imezinduliwa na wagombeaji wa urais, Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga ni chambo cha kunasa kura za Wakenya 2022 kwani haina mantiki yoyote.

Kwanza, chini ya azimio la kukuza uchumi kuanzia mashinani, Dkt Ruto ameahidi kubuni hazina ya Sh150 bilioni, pesa ambazo zitatumiwa kutoa mikopo isiyotozwa riba kwa wafanyabiashara wa kiwango kidogo.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambaye anakimezea mate kiti cha urais, hajasema ni wapi atatoa pesa za kufadhili mpango huo wa kuwapiga jeki walalahoi wala jinsi pesa hizo zitakavyosimamiwa.

Naye Bw Odinga ameahidi kuwageuza wanavijiji kote nchini mamilionea chini ya mwongozo wake wa kuanzisha mageuzi ya kiuchumi katika maeneo ya mashambani, ili kuzuia mtindo wa watu kuhamia mijini.

Mwongozo huu, ambao kwa kiwango fulani unaonekana kushabihiana na ule wa Dkt Ruto, pia unalenga kupiga jeki wafanyabiashara wadogo, kuimarisha uzalishaji wa chakula, utoaji huduma bora ya afya na uimarishaji wa tijara za viwango vidogo vidogo.

Hata hivyo, Bw Odinga hajataja kiwango cha fedha atakazohitaji kufanikisha mpango wake ambao anasema atautekeleza endapo Wakenya watamchagua kuwa rais wa Kenya mwaka ujao.

Sioni kipya ambacho Waziri huyu Mkuu wa zamani anaahidi Wakenya kwa sababu mpango huo alioutangaza pia unafafana na ule uliojulikana kama District Focus for Rural Development ulioasisiwa na rais wa pili wa Jamhuri ya Kenya marehemu Daniel arap Moi katika miaka ya 1990.

Mpango huo wa Moi uliyumbishwa na uongozi mbaya na siasa zilizojikita katika ukabila na uaminifu kwa kilichokuwa chama tawala, KANU, na hatimaye ukafeli.

Ningewaamini Dkt Ruto na Bw Odinga ikiwa wangebainisha mipango ambayo wamefanikisha walipokuwa wakishikilia nyadhifa za chini ili kuonyesha kwamba endapo watapata cheo cha urais wataendeleza kazi hiyo.

Dkt Ruto hasemi ni kwa nini Hazina ya Uwezo iliyoanzisha wakati wa awamu ya kwanza ya utawala wa Jubilee, haijatekeleza malengo yake. Hazina hiyo ilianzishwa na Sh6 bilioni zilizonuiwa kupiga jeki biashara za vijana, akina mama na watu walemavu wakati ambapo Naibu Rais alikuwa na usemi mkubwa serikalini.

Lakini kutokana na usimamizi mbaya wa pesa za hazina hiyo hasa katika ngazi za maeneobunge, imekuwa vigumu kwa walengwa hao kunufaika.

Hii ndiyo maana sasa Dkt Ruto amegeuka na analenga kuwanasa vijana hao wanaoendesha biashara za bodaboda, mama-mboga, waendeshaji mikokoteni miongoni mwa wafanyabiashara wengine wadogo.

Ikiwa usimamizi wa hazina ya Sh6 bilioni ulivurugwa wakati ambapo Naibu Rais alikuwa na ushawishi mkubwa serikalini, siamini kuwa hazina ya Sh150 bilioni anayoahidi kubuni sasa itasimamiwa vizuri.

Vilevile, ikiwa Bw Odinga hakuanzisha sera za kuchochea ustawi wa maeneo ya vijijini alipohudumu kama Waziri Mkuu chini ya serikali ya muungano, ni miujiza gani atakayofanya mwaka ujao endapo ataingia Ikulu?

Isitoshe, kiongozi huyu wa ODM anaahidi kuimarisha uzalishaji wa chakula, uboreshaji wa sekta ya afya atakapoingia Ikulu ilhali hajafanya lolote kufanikisha ndoto hiyo wakati huu ambapo ana usemi katika serikali ya Jubilee kupitia ukuruba wake na Rais Kenyatta.

Kwa hivyo, ninawasihi Wakenya kuwa makini na wachambue miongozo ya wagombeaji urais kwa jicho pekevu.

Waelewe kuwa dhima kuu ya wanasiasa hawa ni kupata kura zao bali sio kuimarisha hali zao za maisha.

You can share this post!

MATHEKA: Serikali inawatesa raia kwa kuongeza ushuru...

Utulivu mdogo Afrika Kusini baada ya jeshi kumwagwa