• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 1:25 PM
Waiguru ahisi huu ni wakati mwafaka wa Jubilee kuzinduka

Waiguru ahisi huu ni wakati mwafaka wa Jubilee kuzinduka

Na SAMMY WAWERU

MGOMBEA wa United Democratic Alliance (UDA) Bw John Njuguna Wanjiku ndiye aliibuka mshindi katika uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge Kiambaa uliofanyika Alhamisi.

Bw Njuguna, almaarufu ‘Kawanjiku’ alizoa kura 21,773 akifuatwa kwa karibu sana na mpinzani wake Kariri Njama wa Jubilee, aliyepata kura 21,263.

Baada ya kutangazwa mshindi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), akiridhia ushindi wake aliutaja kama ushindi wa watu wa Kiambaa.

“Kwanza ni kumshukuru Mungu. Huu ni ushindi wa watu wa Kiambaa. Kwa wapinzani wangu, ninawahimiza tuungane pamoja tufanyie wananchi kazi. Hakuna mshindi wala aliyeshindwa sisi ni watu wamoja Kiambaa,” Bw Njuguna akasema.

Wakati akitangazwa mshindi, ‘Kawanjiku’ alikuwa ameandamana na wabunge wa kundi la ‘Tangatanga’, wakiwemo Kimani Ichungwa (Kikuyu), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Ndindi Nyoro (Kiharu), kati ya wengineo.

UDA inahusishwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto.

Shughuli za kuhesabu kura hata hivyo zilikuwa zimesitishwa kwa muda asubuhi ya kuamkia Ijumaa, Bw Kariri akilalamikia udanganyifu.

Huku ushindi wa UDA Kiambaa ukitafsiriwa kama pigo kwa Rais Uhuru Kenyatta, ngome yake kuvamiwa na Naibu wake Ruto, baadhi ya viongozi na wasiasa kutoka Mlima Kenya wamekiri huenda jamii ya eneo hilo haina furaha na ndio maana inagura Jubilee.

“Kuna uwezekanano wafuasi wa Jubilee hawana furaha. Hatua mahususi na za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili wawache kuondoka chamani,” Gavana wa Kirinyaga, Bi Anne Waiguru akachapisha kwenye kurasa zake za mitandaoni.

Ushindi wa UDA Kiambaa, eneobunge lililoko Kaunti ya Kiambu, wadadisi wa masuala ya kisiasa wanauchambua kuwa ni ishara ya Dkt Ruto kuweza kupenyeza mizizi yake kisiasa eneo la Mlima Kenya na kuwa kipenzi cha wengi, anapochapa kampeni kuingia ikulu 2022.

Kiti cha Kiambaa kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge eneo hilo, Bw Paul Koinange, mnamo Machi 2021.

You can share this post!

Harry Kane haondoki Spurs – kocha Nuno Espirito

ODM yataka msajili atatue mzozo wa fedha wa NASA