• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Wahisani wajitolee kudhamini spoti

TAHARIRI: Wahisani wajitolee kudhamini spoti

KITENGO CHA UHARIRI

NI kweli kwamba kama sekta nyingine, idara ya michezo nchini iliathirika vibaya kutokana na janga la corona takriban miaka miwili sasa.

Kwa kuwa spoti ni sanaa ambayo huhitaji fedha nyingi kama mradi wowote ule, mchezaji awaye yeyote huwa ni sharti ajitimiziwe mahitaji yake ya kimsingi kama mavazi, malazi na makazi safi ndipo apate motisha ya kufanya mazoezi ya mchezo anaoshiriki na hata kufikia kuishinda.

Vivyo hivyo, atahitaji mavazi ya kispoti, mafunzo ambayo yanaendeshwa na wataalamu mahsusi wa spoti anayo kipawa kwayo. Wakati mwingine wachezaji watahitajika kuhudhuria kongamano na warsha tofauti tofauti za kukuza taaluma hizo za michezo yao iwe soka, riadha, handiboli, voliboli, raga na kadhalika.

Kumudu gharama hizi zote huwa si rahisi ndipo wachezaji binafsi hushawishi wahisani wawafadhili ili kujiendeleza na kujinoa.

Klabu kubwa kubwa zilizofanikiwa duniani huwa na ufadhili mkubwa kwa kuwa huwa zinaendeleza shughuli zake bila changamoto zozote. Hii ndio sababu zinashinda kwa urahisi na kupata sifa sufufu. Hili pia hudhihirika kwa wachezaji wa binafsi walio na uwezo wa kifedha.

Majuzi kampuni ya mawasiliano ya Safaricom ilijitolea kumdhamini mtimkaji wa mbio fupi Mark Otieno aliyekuwa akijiandaa kusafiri jijini Tokyo, Japan kwa ajili ya mashindano ya Olimpiki 2020.

Kampuni hii ilikuwa ikiitikia kilio chake ambapo aliomba wahisani wamnunulie viatu vya kisasa ambazo zingeweza kumsaidia ashinde kwa urahisi.

Katika mojawapo wa ripoti zetu leo, mfanyabiashara mmoja wa Mombasa amejitolea kudhamini klabu moja ya soka eneo hilo ili iweze kuinuka na kufikia viwango vya juu vya soka ya kitaifa.

Mhisani huyu pamoja na kampuni ya Safaricom ni mfano wa wanaofaa kupongezwa. Bila shaka kuna kampuni zingine kama EABL, KCB, Equity, Cooperative, ABSA na kadhalika.

Wakati umefika sasa kwa wahisani kujitokeza kusaidia wanamichezo bila ubaguzi hasa wale wa mashinani. Watu binafsi na wanasiasa hawafai kurudi nyuma kuonyesha ukarimu wao katika sekta hii huko vijijini.

Mara nyingi madiwani, magavana na wabunge hutoa ahadi hewa kwa timu za mashambani bila kuzitimiza.

Ni sharti wajue kuwa michezo siku hizi ni kazi na ukuzaji talanta nyumbani kwao kutainua uchumi bali na kuwapa vijana ajira. Ikumbukwe kuwa spoti husaidia kuzima uhalifu na kupunga vitendo vya uhalifu. Kazi kwenu Wasamaria wema!

You can share this post!

Covid: Uhaba wa vitanda, oksijeni waua wengi Afrika

KAMAU: IEBC ijenge imani ya uwajibikaji miongoni mwa Wakenya