• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
KAMAU: IEBC ijenge imani ya uwajibikaji miongoni mwa Wakenya

KAMAU: IEBC ijenge imani ya uwajibikaji miongoni mwa Wakenya

Na WANDERI KAMAU

KWA miaka yote ambapo ghasia za baada ya uchaguzi zimeshuhudiwa nchini tangu uhuru, moja ya sababu kuu zimekuwa ni tume za uchaguzi ambazo zimekuwepo.

Tume hizo zimekuwa zikielekezewa kila aina ya lawama; kuu likiwa kuonyesha mapendeleo kwa baadhi ya mirengo ya kisiasa.

Lawama nyingine imekuwa ni madai ya wizi wa kura za mirengo pinzani, ili kuusaidia upande wa kisiasa unaopendelewa na serikali.

Kwa urejeleo wa kina, tuhuma hizo ndizo zilisababisha ghasia zilizoshuhudiwa nchini mnamo 1992, 1997, 2007 na 2017.

Kwenye chaguzi kuu za 1992 na 1997, Tume ya Uchaguzi Kenya (ECK) ililaumiwa kwa kumpendelea marehemu Daniel Moi, ikizingatiwa ndiye aliyekuwa Rais.

Kwenye uchaguzi wa 1992, wagombea wakuu wa urais kama Jaramogi Oginga Odinga (Ford-Kenya), Rais Mstaafu Mwai Kibaki (DP), marehemu Kenneth Matiba (Ford-Asili) kati ya wengine walidai kuwa Moi alitumia ushawishi wake kuathiri matokeo ya uchaguzi huo, ambapo alitangazwa kuwa mshindi.

Vivyo hivyo, madai hayo yalitolewa kwenye uchaguzi wa 1997, ambapo vigogo wao hao, wakiwemo Bw Kibaki na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, walidai kuwa serikali ilitumia nguvu zake kuhakikisha Mzee Moi alitwaa ushindi.

Hali ilidorora kwenye uchaguzi wa 2007, ambapo aliyekuwa mwenyekiti wa ECK, marehemu Samuel Kivuitu, alisema hakujua aliyeibuka mshindi kati ya Mabwana Kibaki na Odinga.

Matamshi hayo ndiyo yanayodaiwa kuchangia kuongezeka kwa taharuki ya kisiasa iliyojengeka nchini, ambayo hatimaye iligeuka kuwa moja ya machafuko mabaya zaidi ya kikabila kuwahi kushuhudiwa nchini.

Baada ya matamshi hayo, ODM ilimtaja Bw Odinga kuwa mshindi wa urais, huku PNU ikishikilia Bw Kibaki ndiye alikuwa mshindi halali wa uchaguzi huo.

Bila shaka, matukio hayo yanadhihirisha kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ina kibarua kikubwa katika kuhakikisha inajenga imani ya uwajibikaji miongoni mwa Wakenya, hasa nchi inapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Juhudi zinapoendelea kuwasaka makamishna wapya kujaza nafasi zilizo wazi katika tume hiyo, lazima wale watakaoteuliwa wafahamu kuwa vitendo vyao ndivyo vitakapoamua mwelekeo na mustakabali wa nchi baada ya uchaguzi huo.

Lazima wajue kuwa mustakabali wa Kenya umo mikononi mwao wanapoendesha uchaguzi huo.

Kijumla, wito wetu ni kwa IEBC kuendelea kulainisha matayarisho yake ili kuondoa vikwazo vilivyoshuhudiwa hapo awali.

Jukumu lake linafanana na rubani anayewabeba mamia ya abiria kwenye ndege ikiwa angani.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Wahisani wajitolee kudhamini spoti

MUTUA: Mbona hasira za Wakenya zinaishia kuuana kiafriti?