• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:55 PM
AKILIMALI: Mkulima wa miche ya mimea asilia aliyekita kambi jijini Nairobi

AKILIMALI: Mkulima wa miche ya mimea asilia aliyekita kambi jijini Nairobi

Na SAMMY WAWERU

LAVINGTON ni mtaa wa kifahari jijini Nairobi na wenye shughuli chungu nzima za kimaendeleo.

Ni katika mtaa huo tunakutana na Wilson Ndung’u, ambaye ni mmoja wa jamii ya ‘wakazi’.

Ndung’u ni mkulima. Ni mkulima wa aina yake jijini.

Wengi watashangaa anavyoendeleza kilimo katika mazingira yasiyo na ekari za mashamba, ila majengo ya biashara na makazi pekee.

Pembezoni mwa barabara kuu inayoelekea mtaa wa Lavington, Ndung’u ana kiunga cha miche ya mimea asilia.

Ni wengi jijini Nairobi wamekumbatia ukuzaji wa miche ya matunda na maua kandokando mwa barabara, lakini barobaro huyu ana upekee.

Ndio huzalisha miche, ila ni ya mimea ambayo ni vigumumu kuipata nchini.

“Miche ninayokuza ni mimea asilia na yenye asili ya nchi za ng’ambo,” asema.

Anafichua kwamba, kando na kuwa asilia ni dawa.

“Hutumika kutengeneza dawa za kienyeji, na mingine inatumika ilivyo kama dawa, kuimarika kinga ya mwili dhidi ya magonjwa,” aelezea.

Isitoshe, imesheheni madini na virutubisho faafu katika mwili wa binadu.

“Ukiingia katika baadhi ya mikahawa na hoteli jijini, uagize kinywa-dawa, hutokana na baadhi ya mimea ya miche ninayokuza,” anasema.

Miche hiyo inajumuisha Vanilla, Chamomile, Dandelion, Lemon Verbena, Mugwort, Rue, Tribulus terrestris, Hadjod, Ajuga remota kati ya mingineyo mingi.

Ndung’u anafichua, inapokomaa, baadhi huiongeza thamani kwa kutengeneza unga wa vinywaji.

Mbali na miche hiyo, Ndung’u pia hulima ya matunda kama vile Brazilian grapes, Nectarine, Lychee na Kaki.

“Ni matunda yasiyopatikana huyu nchini, nitaridhia taifa likiyakumbatia,” anasema.

Yanayopatikana, labda kwenye maduka ya jumla na ya kifahari, bei yake ikiwa haikamatiki.

Safari ya kufika aliko sasa, ilianza 2019.

Ndung’u anasimulia, kabla ya kuchukua hatua ya kuwa mkuzaji wa miche ya mimea asilia na anayoitaja kuwa ya busara, alikuwa muuzaji wa matunda kijumla.

“Baada ya kufanya mtihani wa kidato cha nne KCSE 2012, niliingilia uuzaji wa mseto wa matunda kwa maduka ya jumla,” aelezea.

Wilson Ndung’u akionyesha mche wa mmea asilia aina ya Vanilla, katika kiunga chake eneo la Lavington, Nairobi. Picha/ Sammy Waweru

Ni katika harakati za kulisha taifa matunda, aligundua kuwepo kwa gapu ya miche anayokuza, nchini.

Kamwe hajutii uamuazi wake, kwani ndiyo kazi iliyomuajiri. “Ratiba yangu kuanzia asubuhi mpaka jioni huwa hapa kiungani,” akasema wakati wa mahojiano ya kipekee eneo la Lavington.

Mwanamazingira huyu alisema shabaha yake ni kuona watu wamerejelea mimea asilia, ili kusaidia kero ya magonjwa kama vile Saratani.

Safari kuimarisha kiunga chake hata hivyo haijakuwa rahisi.

“Miche ya mimea ninayokuza inahitaji maji mengi na safi, ningali ninategemea maji ya mvua. Uhaba wa maji wakati mwingine huwa ni kikwazo,” anasema.

Daniel Mwenda, mtaalamu wa masuala ya matunda na miti anasema ufanisi katika kilimo cha matunda unategemea kuwepo kwa maji.

“Ukulima wa matunda unafanikishwa na kuwepo kwa maji ya kutosha, hivyo basi ni muhimu mkulima ajiendae ipasavyo kwa vyanzo vya raslimali hii,” Mwenda anashauri.

Aidha, mdau huyu anahimiza haja ya kukumbatia mfumo wa uvunaji maji kupitia vidimbwi na mabwawa.

“Isitoshe, mfumo wa unyunyiziaji mimea na mashamba maji kwa mifereji (Irrigation) ndio bora zaidi,” asisitiza.

You can share this post!

Kiungo Felipe Anderson arejea Lazio baada ya kuagana na...

Fainali ya UEFA 2023 sasa kuandaliwa Istanbul kutokana na...