• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
Miaka 10 baada ya ugonjwa wa Rinderpest kuondolewa duniani, ulitokomezwa vipi?

Miaka 10 baada ya ugonjwa wa Rinderpest kuondolewa duniani, ulitokomezwa vipi?

Na  SAMMY WAWERU

COVID-19 imeonyesha si rahisi kukabili na kutokomeza ugonjwa hasa ule ambukizi kupitia virusi.

Hata hivyo, kupitia tafiti za wataalamu, Wanasanysi, madaktari na wadau husika, inawezekana.

Ni kufuatia hilo, ulimwenguni maradhi mawili pekee ya mifugo yamethibitishwa kutokomezwa

Rinderpest, ugonjwa hatari wa mifugo na wanyamapori ulitokomezwa kutoka uso wa ulimwengu 2011.

Vilevile, ugonjwa wa Smallpox na ambao uliathiri binadamu ulitokomezwa mwaka wa 1980.

Kulingana na watafiti, Rinderpest ilikuwa ugonjwa wa kitambo ulioathiri mifugo wa nyumbani na wanyamapori.

Dalili zake zilikuwa kiwango cha juu cha joto, mifugo kukosa hamu ya kula, kusokotwa na tumbo, kuhara na kuwa na vidonda mdomoni.

Aidha, dalili zingine ni pamoja NA maumivu sehemu za haja, ukosefu wa nguvu na hatimaye mnyama aliyeugua kufariki kati ya siku 6 – 12.

Ufanisi kuutokomeza, tasisi ya kwanza na maalum ya masuala ya mifugo ilizinduliwa katika Chuo Kikuu cha Lyon France mwaka wa 1762, kufanya tafiti.

Chanjo ya Rinderpest ilikuwa ya kwanza kutengenezwa nchini Kenya, ili kuukabili.

“Tulifanikiwa kuutokomeza kupitia utoaji chanjo kwa mifugo Baranai Afrika,” anasema Dkt Walter Masiga, mmoja wa watafiti African Union Inter-African Bureau for Animal Resources (AU IBAR).

Kupitia Pan-African Rinderpest Campaign (PARC) iliyoshirikiana na AU IBAR,Kenya ilikuwa miongoni mwa mataifa 34 yaliyohusika.

“Tulifanikisha mikakati tuliyoweka kupitia ushirikiano wa karibu na viongozi wa kisiasa,” Dkt Masiga aelezea.

Kulingana na mdau huyu, mpango huo pia ilishirikisha taasisi za kimataifa kama vile; Food and Agriculture Organization (FAO), The World Organization for Animal Health (OIE) na UNICEF, ambapo kila mhusika alitoa mapendekezo na mchango wake.

Kisa cha mwisho cha Rinderpest kiliripotiwa Kenya mnamo 2001. Kati ya 2002 hadi 2011, hakuna kisa kilichoripotiwa.

“Kilele kilikuwa 2011 OIE ilipotangaza Rinderpest imetokomezwa,” Dkt Masiga adokeza.

Mwaka wa 2010, FAO ilikuwa na imani kuwa virusi vya Rinderpest vilikuwa vimetokomezwa kabisa, mbali na vilivyohifadhiwa kwenye maabara.

Safari hiyo hata hivyo haikuwa rahisi.

Dkt Dickens Chibeu aliyeongoza kitengo cha utafiti cha Epidemiological, katika Shirika la Mifugo Nchini (DVS), anasema walifanya kazi kwa bidii kushawishi maafisa na madaktari wa mifugo, kuzingatia utoaji chanjo.

“Tuliweza kuibuka na kitengo cha utafiti, epidemiological, ili kusaidia kudhibiti hali,” Dkt Chibeu anasema.

Mtafiti huyu anasema baadaye alifanya kazi na Somali Ecosystem Rinderpest Eradication Coordination Unit (SERECU), kama mshirikishi wa AU IBAR.

Dkt Chibeu anasifia mpango wa SERECU katika oparesheni kusaidia kutokomeza Rinderpest.

“Ukosefu wa usalama hata hivyo ni miongoni mwa changamoto tulizopitia. Lengo letu hasa lilikuwa kukabili Rinderpest, na kuitokomeza kabisa na kupitia ushirikiano wa viongozi wa kisiasa na serikali tulifanikiwa,” afafanua.

Huku 2021 ulimwengu ukiadhimisha miaka 10 ya kutokomeza Rinderpest, nchi zinazoendelea kuhifadhi vifaa vilivyotumika zinazua hatari ya uwezekano wa mlipuko wa ugonjwa huo hatari ulioangamiza mifugo.

Yote tisa, kumi ikiwa Rinderpest iliondolewa, Covid-19 ugonjwa ambao ni janga la kimataifa, pia unaweza kutokomezwa.

You can share this post!

Chelsea waanza kujiandaa kwa msimu mpya wa 2021-22 kwa...

Je tutajifunza lini?