• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:55 AM
Majumba ya kifahari yalivyogeuka maficho ya uhalifu utalii ukidorora

Majumba ya kifahari yalivyogeuka maficho ya uhalifu utalii ukidorora

Na ALEX KALAMA

MAJUMBA ya kifahari yaliyokuwa yakitumiwa na watalii mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi, yamebaki magofu.

Baadhi sasa yanatumika kama maficho ya wahalifu baada ya sekta ya utalii kukumbwa na changamoto tele.Kwa miaka mingi, mji wa Malindi ulikuwa ukitambulika kimataifa kama kivutio kikuu cha utalii eneo la Pwani.Kutokana na mandhari yake ya kupendeza na mji kuwa safi na hali nzuri ya hewa, watalii wengi walivutiwa kuzuru Malindi.

Yote hayo yalifanikishwa kwa sababu ya ushirikiano mzuri kati ya vitengo vya usalama, wafanyabiashara, viongozi na maafisa wa baraza la mji. Kulikuwa na mipango bora iliyowekwa kuhakikisha mji unakuwa safi kimazingira na imara katika miundomsingi.

Kutokana na sifa hiyo uchumi wa mji ulikua na kuvutia mno wawekezaji wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali barani Ulaya, waliotua nchini kuja kufanya biashara katika mji wa Malindi.Enzi hizo wageni walifurika katika hoteli za kifahari kama Eden Rock, Sin Bird, Blue marlin, Sea view Resort, Double Heart Resort, Coral Key, Kivulini, Coconut Village, Tamani Jua Resort, SuliSuli, Palm Tree, African Pearl, Lion the Sun, Dream of Africa na Lawfords.

Ustawishaji huu wa utalii ulichangia pakubwa kuunda nafasi tele za ajira.Hata hivyo, baada ya ustawi huo hali sasa imebadilika kuwa tofauti kabisa.Kaunti ya Kilifi ilikuwa mojawapo ya zile za Pwani zilizoanza kuathiriwa mno kitalii baaada ya mashambulizi ya kigaidi kuanza kushuhudiwa nchini mara kwa mara katika miaka ya hivi majuzi.

Visa hivyo vilifanya baadhi ya mataifa ya ng’ambo kuonya raia wake dhidi ya kutembelea Kenya kiholela; hali iliyosababisha idadi ya watalii wanaozuru nchini kupungua mno.Hilo pamoja na changamoto zingine kama vile ghasia za baada ya uchaguzi na la hivi punde la janga la corona, zimesababisha kudorora mno kwa sekta ya utalii.

Hoteli nyingi zimefungwa mjini Malindi kwa kukosa wageni.Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa, baadhi ya hoteli na majumba ya kifahari yaliyokuwa yakitumiwa kwa utalii sasa yamesalia kuwa magofu yanayotumiwa na wahalifu.

Hii ni baada ya wamiliki kuyafunga sababu ya kutokuwepo kwa wateja, jambo ambalo pia limewaacha maelfu ya wakazi kukosa ajira.Wadau wa utalii Malindi wanahofia huenda sekta hiyo ikasambaratika kabisa endapo watalii hawatahakikishiwa usalama wao katika eneo hilo.

Mwanaharakati wa kijamii eneo hilo, Bw Stembo Kaviha, ameitaka serikali ya kaunti kuyakagua majumba ambayo yamesalia kuwa magofu, na kuyabomoa.Alieleza kwamba kuna hofu kubwa kwamba majumba hayo yataendelea kutumiwa na wahalifu, hivyo kuwa tishio la usalama.

“Tunachotaka ni serikali ya kaunti iwatafute wanaomiliki majumba haya wayarekebishe ili yaweze kutumika tena. Aidha, ikiwa hawataweza kuyafanyia ukarabati basi kaunti iyanunue na kuyarekebisha ili biashara ya hoteli ifufuliwe na watu waajiriwe.

Iwapo hilo pia haliwezekani, basi yabomolewe badala ya kuachwa hivyo kwani wahalifu wamepata mahali pa kujificha ambapo hutokea usiku kututatiza,” alieleza Bw Kaviha.Kulingana na maneja wa klabu ya mpira wa gofu mjini Malindi, Bw Anthony Deche, uhalifu sasa umeibuka kuwa changamoto nyingine itakayoanza kuwaingiza hofu watalii wachache waliobaki mjini humo.

“Utovu wa usalama eneo hili umechangiwa zaidi na vijana ambao wamejitumbukiza katika uraibu wa mihadarati na ulevi. Hii imewafanya watalii kuogopa sana,” alisema Bw Deche.Ni kauli ambayo iliungwa mkono na aliyekuwa meya wa mji wa Malindi, Bw Samson Mapinga.“Wajua mgeni hawezi kuja sehemu ambayo hayuko huru.

Yeye anatakapahali ambapo atatalii bila wasiwasi. Wageni hawataki kuhangaishwa kimawazo; wamekuja kustarehe. Visa hivi vya uhalifu ndivyo vinazidi kuwatia woga,” akasema Bw Mapinga.Afisa Mkuu wa Polisi eneobunge la Malindi, Bw John Kemboi, alithibitisha kwamba kumeshuhudiwa visa ambapo majumba ya kifahari yaliyotelekezwa yanatumiwa kama maficho ya washukiwa wa uhalifu eneo hilo.

Alitoa mfano wa kisa cha mwishoni mwa mwezi Mei ambapo kijana mmoja alipatikana amelala katika moja ya majumba hayo bila idhini.Alikamatwa na kufikishwa kortini kwa kushukiwa kuhusika katika uhalifu.Bw Kemboi alihakikishia wadau katika sekta ya utalii na jamii kwa jumla kwamba idara ya polisi imeweka mikakati mwafaka ili kudumisha usalama Malindi.

Kulingana naye, baadhi ya mikakati itatekelezwa kwa ushirikiano na kitengo cha polisi wa kuwalinda watalii, ambacho jukumu lake ni kutoa ulinzi kwa watalii pamoja na mali zao.Mkuu huyo wa polisi alieleza kwamba tangu kuundwa kwa kitengo hicho hakujakuwa na visa vya usalama vinavyolenga watalii.

“Jukumu la idara ya polisi ni kuhakikisha kuna amani na usalama. Miongoni mwa mikakati iliyowekwa na idara ni kuundwa kwa kitengo maalum cha kulinda watalii na mali zao,” alihoji.Kwa upande wake, afisa wa utalii katika serikali ya Kaunti ya Kilifi, Bw William Iha, alisisitiza kuwa licha ya utalii kufifia eneo hilo, anaamini kuwa sekta hiyo inaweza kufufuliwa na hoteli kufunguliwa tena.

Aidha, Bw Iha, alieleza kuwa jambo la msingi ni kuweka mikakati ya kupambana na changamoto zilizopo ili kufahamu jinsi ya kukabiliana nazo.Miongoni mwazo ni kuwashirikisha wakurugenzi wa hoteli katika vikao vya kujadili ufufuzi na ustawishaji tena wa utalii, kushirikiana na hazina ya utalii nchini ambayo ina mchango mkubwa kufadhili harakati za ufufuzi, na pia kushirikisha wadau wote wakubwa kwa wadogo katika mchakato mzima.

Vilevile, alisema Kaunti ya Kilifi inafaa kujenga majumba na kumbi za kisasa za mikutano au makongamano.Hii ni mojawapo ya mikakati ibuka ya kutandua chambo cha kunasa watalii, lengo likiwa kuwavutia wawekezaji mbalimbali kuzuru mji huo wanapohudhuria makongamano hayo.

  • Tags

You can share this post!

Waathiriwa 800 wa mkasa wa moto na mafuriko katika wodi ya...

Mama aomba korti imnyime dhamana mwanamme aliyewapiga...