• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 1:35 PM
Mwana habari na mwigizaji chipukizi anayepania kuzidisha umaarufu

Mwana habari na mwigizaji chipukizi anayepania kuzidisha umaarufu

Na JOHN KIMWERE

INGAWA hajapiga hatua kubwa anasema amepania kujituma kisabuni ili kuhakikisha ameibuka kati ya wasanii mahiri katika sekta ya uigizaji duniani.

Alice Njeri Muthoni ni mwana habari na mwigizaji chipukizi anayepania kufuata nyayo za mwigizaji wa filamu za Hollywood, Priyanka Chopra mzawa wa India aliyejizolea umaarufu kupitia filamu kama ‘Quantico,’ na ‘White Tiger’ kati ya zingine. Kipusa huyu ni mwana habari katika kituo cha Redio cha Bus Radio Sauti ya Kajiado katika Kaunti ya Kajiado.

RIWAYA

Dada huyu ambaye pia kisanaa anafahamika kama Alice kwenye filamu za steji shoo ambazo huigiza kwa kufuata mwongozo wa vitabu za riwaya (Set Books). ”Maana ninahisi nina kipaji, mwanzo wa ngoma nimepania kujijenga katika uigizaji wa filamu zinazotosha mboga kupeperushwa kwenye runinga za kitaifa.

Ingawa bado sijapata mashiko katika tasnia ya filamu nchini uigizaji umekuwa tegemeo langu ndani ya miaka kadhaa iliyopita kabla sijaanza kibarua cha uanahabari mwaka huu,” binti huyu anasema na kuongeza kuwa sekta ya uigizaji imeajiri watu wengi nchini.

 Picha /JOHN KIMWERE
Mwigizaji chipukizi Alice Njeri Muthoni.

Msichana huyu alianza kujituma katika masuala ya uigizaji mwaka 2012 baada ya kukamilisha elimu ya sekondari. Anajivunia kufanya kazi na makundi kadhaa ikiwamo Jicho 4 Productions, Forever Arts Group na Liquids Art Entertainment.

LUPITA NYONG’O

”Nikiwa mtoto nilitamani kuhitimu kuwa mwana habari pia mwigizaji ambapo katika tasnia ya maigizo kazi na ukakamavu wake Lupita Nyong’o Mkenya anayetamba katika filamu za Hollywood ulinitia moyo zaidi,” akasema.

Anaongezea kuwa kujituma kwake kulimzawadi tuzo ya Oscar iliyomtia motisha zaidi. Kadhalika anadokeza kuwa Lupita ameibuka kivutio kikubwa kwa waigizaji wanaokuja hapa nchini.Chipukizi huyu anajivunia kushiriki filamu moja iitwayo ‘Kihiko'(Harusi) iliyopata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga ya mtandaoni kwa jina Thingira TV.

Kwa wasanii wa Afrika dada huyu angependa kufanya kazi na waigizaji kama Gennevieve Nnaji wa Nigeria (Blood Sisters,’ ‘Lion Heart). Pia yupo mwigizaji wa Tanzania, Jacqueline Wolper ambaye ameshiriki filamu kama ‘Red Valentine,’ na ‘Family Tears,’ kati ya zingine.

KUNOA

”Bila mapendeleo wala kuongeza kachumbari sekta ya filamu hapa Kenya inayo nafasi nzuri kupiga hatua tena zaidi na kufaidi wasanii wengi wanaume kwa wanawake,” alisema na kuongeza kuwa hata hivyo inahitaji kufanyiwa kazi kubwa hasa katika uwekezaji.

Pia anasema kuna umuhimu mkubwa kwa waigizaji chipukizi kutambuliwa na kuanza kunolewa makali yao wakiwa wadogo kama ilivyo katika mataifa yanayoendelea. Kuhusu masuala ya mahusiano anasema ”Kwa sasa nipo singo lakini sitaki kuingia katika mahusiano hivi karibuni.

Wanaume wamenivunja moyo mara kadhaa ambapo kiasi nimeamua kupiga breki nijijenge kwanza.” Anahimiza wasanii chipukizi kuwa wasivunjike moyo kwa kukosa ajira mbali wazidi kujituma wanapopata nafasi ya kuonesha uwezo wao na waamini ipo siku Mungu atafungua milango ya mafanikio.

  • Tags

You can share this post!

Wasichana wa Mukuru Talent wakata tikiti ya fainali

Mwigizaji anayepania kutinga upeo wa kimataifa