• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 12:47 PM
Tuchukue mkopo kufungua nchi – Raila

Tuchukue mkopo kufungua nchi – Raila

ANTHONY KITIMO na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga ametaka serikali ichukue mikopo zaidi itakayogharamia chanjo ya kuepusha maambukizi ya virusi vya corona ili nchi ifunguliwe.

Alisema hayo jana alipomtaka Rais Uhuru Kenyatta afungue nchi ili uchumi uanze kustawi baada ya kuathirika na janga la corona kwa zaidi ya mwaka mmoja.Akizungumza jana katika Kaunti ya Mombasa, Bw Odinga alisema Kenya iko hatarini kupiga hatua kubwa nyuma kimaendeleo ikiwa baadhi ya masharti makali ya kuepusha ueneaji wa virusi vya corona hayatalegezwa.

Masharti hayo ni kama vile kafyu inayozuia raia kutoka nje usiku na sheria za kuzuia mgusano wa watu ambazo zimesababisha hasara kwa sekta mbalimbali kama vile za uchukuzi na hoteli.“Tunataka zile dawa hata kama zinagharimu pesa ngapi, pesa zitolewe hata kama zinakopwa tukope, hata wabunge wakipandisha kiwango tunachoweza kukopa bora chanjo ije.

Pesa pia ipeanwe kwa mama mboga na vijana wetu, ili wananchi wapate pesa mfukoni,” akasema.Alikuwa akihutubu katika warsha ya kusherehekea Eid-Ul-Adha iliyoandaliwa na Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir katika ukumbi wa Bhadalla.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Mbunge wa Likoni Mishi Mboko, mwenzake wa Kipipiri Amos Kimunya, madiwani miongoni mwa wageni wengine walioalikwa.

Bw Odinga alisema nchi inahitaji kutoa chanjo kwa angalau watu milioni 15 ili ifuate mwelekeo wa mataifa ambayo yameanza kurudia hali ya kawaida, ilhali kufikia sasa ni watu milioni 1.6 pekee waliopokea chanjo hiyo.

“Wakati huu tuko na shida kwa sababu ya hili janga la corona. Corona imeporomosha uchumi na kuna shida nyingi. Biashara nyingi zimekufa, kuna ukosefu wa kazi na njaa. Namshauri ndugu yangu Uhuru Kenyatta achukue hatua,” akasema.

Ijapokuwa mamilioni ya raia wanatatizika kwa makali ya athari za Covid-19 kwa uchumi, serikali tayari imechukua mikopo mingi ambayo yalipita Sh7 trilioni, kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Kenya (CBK).Hii imelazimu wananchi kulipa kiasi kikubwa cha ushuru kwa bidhaa wanazotegemea kila siku ili kuwezesha serikali kugharamia madeni yake kwa nchi za kigeni kama vile China.

Madeni hayo yamewaongeza raia mzigo licha ya kuwa wengi tayari wanalemewa kiriziki baada ya corona kuzorotesha uchumi.Wito wa kutaka masharti yanayohusu Covid-19 yalegezwe ulianza kutolewa na Bw Joho, ambaye alieleza masikitiko kuhusu jinsi biashara kama vile za mabasi ya uchukuzi na matatu zinavyoathirika.

‘Ni wakati sasa tufungue uchumi wa kitaifa kikamilifu ili watu wapate kazi. Mabasi yanafungwa, matatu zinasota. Serikali itafute pesa kila mtu apate chanjo ili kila mtu awe huru kutembea bila wasiwasi lakini uchumi ufunguliwe kikamilifu,’ akasema Bw Joho.

Hivi majuzi, baadhi ya makampuni yalithibitisha kusitisha uchukuzi wa umma kwa sababu ya hasara zinazotokea wanapolazimika kubeba nusu ya idadi ya kawaida ya abiria.Hatua hiyo imesababisha ongezeko la ukosefu wa ajira kwa idadi kubwa ya wananchi waliokuwa wameajiriwa kuhudumu katika mabasi hayo, na wale waliotegemea abiria kwa biashara zao katika vituo mbalimbali barabarani.

  • Tags

You can share this post!

Ndege iliyobeba abiria 40 yatua ghafla

Kiongozi wa upinzani TZ azuiliwa usiku wa manane