• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Kiongozi wa upinzani TZ azuiliwa usiku wa manane

Kiongozi wa upinzani TZ azuiliwa usiku wa manane

Na CITIZEN

KIONGOZI wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, jana alikamatwa pamoja na wanachama wengine wakienda kufanya mkutano kuishinikiza serikali kufanya mageuzi ya kikatiba.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na chama hicho, Freeman Mbowe alikamatwa na watu wengine kumi katika mji wa Mwanza usiku wa manane.“Tunakashifu mtindo wa serikali kukiuka haki za Watanzania kwa kutumia nguvu.

Hizi ni ishara kuwa uongozi wa kidikteta bado unaendelea kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa marehemu John Magufuli.“Freeman Mbowe alikamatwa na polisi mara tu baada ya kufika katika hoteli moja mwendo wa saa 8.30 alfajiri.

Alikamatwa pamoja na viongozi wengine,” kilieleza Chadema.Ijapokuwa wanachama wengine walipelekwa katika kituo cha polisi cha Mwanza, haijabainika aliko kiongozi huyo.“Tunawataka polisi kujitokeza wazi kueleza aliko mwenyekiti wetu na sababu za kukamatwa kwake,” kikaongeza.

Kukamatwa kwa kiongozi huyo kunajiri miezi minne baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua uongozi mnamo Machi, kufuatia kifo cha Rais Magufuli.Kumekuwa na matumaini miongoni wa raia kuwa Rais Suluhu atabadili mtindo wake wa uongozi kwa kuruhusu uhuru wa kujieleza, ikilinganishwa na mtangulizi wake.

Magufuli alipewa jina la msimbo “Bulldozer” kutokana na ukakamavu mkuu aliodhihirisha wakati wa uongozi wake. Lakini baadhi ya watu walimkosoa kwa kuendeleza “udikteta” na “kutowavumilia wapinzani.

”Mbowe alikamatwa baada ya kuapa kuandaa mkutano maalum kuhusu mageuzi ya kikatiba, licha ya maafisa wa serikali mkoani Mwanza kupiga marufuku mikusanyiko ya umma ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

“Hatuwezi kuendelea kwa mtindo wa zamani,” akasema Mbowe kwenye video iliyopachikwa katika mtandao wa kijamii wa Twitter mnamo Jumatatu.“Tuna haki ya kukutana japo huwa tunakamatwa, kupigwa, kufunguliwa mashtaka, kufikishwa kortini kwa muda halafu baadaye tunaachiliwa huru.

Ikiwa wanataka kukamata wanachama wote wa Chadema, basi kwanza wapanue magereza kwani sote tuko tayari kukamatwa. Hatutaitisha dhamana,” akasema.Mnamo Aprili, Rais Suluhu alifanya kikao na upinzani akaahidi kutetea demokrasia na haki za msingi za raia.

Novemba iliyopita viongozi kadhaa wa upinzani akiwemo Mbowe walizuiliwa kwa muda, baada ya kuitisha maandamano dhidi ya kile walichodai kuwa “wizi wa kura” katika uchaguzi mkuu ambao Rais Magufuli alitangawa mshindi na kuanza kuhudumu kwa muhula wa pili.

Rais Magufuli alifariki mnamo Machi baada ya kudaiwa kukumbwa na maradhi ya moyo. Hata hivyo, wapinzani wake walidai alifariki kutokana na virusi vya corona.

  • Tags

You can share this post!

Tuchukue mkopo kufungua nchi – Raila

Wahamiaji wazidi kufurika Uingereza