Magoha azindua mpango wa kutoa msaada wa masomo kwa watoto kutoka jamii masikini

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Elimu Profesa George Magoha Alhamisi aliwazindua watahiniwa 9,000 wa mtihani wa KCPE, 2020 ambao wamefaidi kutoka mpango wa msaada wa  msaada wa masomo unaofadhiliwa na serikali kuu kwa ushirikiano na Benki ya Dunia.

Wanafunzi hao kutoka familia masikini kutoka mashambani na katika mitaa ya mabanda ni miongoni  wa zaidi ya wanafunzi 45,000 waliotuma maombi ya msaada huo.

Akiongea katika hafla ya iliyofanyika katika ukumbu wa Taasisi ya Kuandaa Mtaala Nchini (KICD) Profesa Magoha alisema kuwa msaada huo, maarufu kama, “Elimu Scholars Programme” utagharamia mahitaji yote ya wanafunzi hao kwa miaka minne.

“Msaada huu wa masomo ni kamilifu. Wanafunzi hawa watalipiwa karo zote, nauli na kupewa fedha za matumizi kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne. Hii ni kuanzia mwaka huu wa masomo unaoanza Jumatatu, Julai 26,” akaeleza.

Profesa Magoha ambaye alikuwa amendamana na Katibu katika Wizara hiyo ya Elimu Dkt Julius Jwan alisema kuwa japo idadi ya wanafunzi walioteuliwa ni ndogo ikilinganishwa na wale waliotuma maombi, uteuzi wao uliendeshwa kwa njia huru na haki.

Shughuli ya uteuzi wa wanafunzi hao 9,000, akaongeza, iliendeshwa chini ya mfumo unaozingatiwa chini ya mpango wa msaada wa masomo wa “Wings to Fly” unaofadhiliwa na Wakfu wa Benki ya Equity.

“Kwa hivyo, ningependa kushukuru zaidi Mkurugenzi Mkuu wa Wakfu wa Benki ya Equity James Mwangi kwa msaada waliotupa katika uteuzi wa wanafunzi hawa. Lakini shukrani zaidi ziendee mwenzangu Waziri wa Usalama Fred Okeng’o Matiang’i kwani kupitia msaada wa machifu na manaibu wao tuliweza kuingia vijijini na katika mitaa ya mabanda na kuwatambua watoto wenye werevu wenye mahitaji maalum,” akaeleza Profesa Magoha.

Waziri alisema walioteuliwa ni wale watahiniwa waliopata kuanzia alama 288 kwenda juu katika mtihani huo wa KCPE na ambao wameratibiwa kujiunga na kidato cha kwanza kuanzia Agosti 2, mwaka huu.

Profesa Magoha alisema wanafunzi hao 9,000 ni kundi la pili la wanafunzi ambao kufikia sasa wamefaidi chini ya mpango huo wa “Elimu Scholars Programme”. Kundi la kwanza la wanafunzi 9,000 lilizinduliwa mwaka jana na sasa watajiunga na kidato cha pili juma lijalo.

“Dhima kuu ya mpango huu ulioasisiswa na Rais Uhuru Kenyatta ni kuhakikisha kuwa watoto kutoka familia masikini wanapata nafasi ya kuendelea na masomo. Huu ni wajibu mkuu wa serikali kuu kwa mujibu wa katiba na unaenda sambamba na sera iliyoanzishwa na Rais ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaofanya mtihani wa KCPE wanajiunga na shule za upili,” akaeleza.

Kadhalika Profesa Magoha alitoa wito kwa mashirika mengine kutoa misaada kama hiyo kwa wanafunzi kutoka jamii masikini lakini ambao ni werevu huku akipongeza mpango wa Wings to Fly.

“Nitazungumza na rafiki yangu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kenya Commercial Joshua Oigara ili atoe msaada wa masomo kwa angalau wanafunzi 200.Wabunge walitumie sehemu ya Hazina ya CDF kufadhili masomo ya wanafunzi kutoka jamii masikini. Serikali za kaunti pia zisiachwe nyuma katika harakati hizi za kuwasaidia watoto wetu,” akaeleza.