Dereva asimulia jinsi alivyookoa abiria basi lilipovamiwa na magaidi

SIAGO CECE na FARHIYA HUSSEIN

HEBU tafakari kuhusu hali ambapo unakumbana na shambulio la kigaidi ambalo nusura litamatishe maisha yako.

Hata hivyo, lazima utumie njia lilikotokea, kwa kusafiri umbali wa kilomita 300 kila siku. Abdul Abdalla, 41, ni dereva wa basi.

Amekuwa akisafiri kati ya miji ya Lamu na Mombasa kwa muda wa miaka 12.Hata hivyo, hana mipango ya kuacha kazi yake, licha ya kuwa miongoni mwa madereva ambao wamekumbana na mashambulio hatari zaidi ya kigaidi.

Alinusurika kwenye shambulio la basi katika barabara ya Lamu-Witu-Garsen na lile la Mpeketoni mnamo 2014, ambapo mamia ya watu waliuawa.

“Walifyatulia risasi basi nililokuwa nikiendesha mara tano katika kioo kilicho katika eneo la dereva. Ni kama walikuwa wakilenga kuharibu magurudumu. Wakati huo wote, nilikuwa nimeangalia chini. Baadaye, nilianza kupunguza mwendo. Ikiwa singefanya hivyo, wangetuua sisi sote,” akasema Abdalla.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Abdalla anaeleza kuwa siku hiyo, alikuwa ameondoka Mombasa mwendo wa saa nne asubuhi, akiwa amewabeba abiria 62 katika basi la Kampuni ya Mabasi ya Tawakal. Alikuwa akielekea Lamu.

“Nilifika Malindi mwendo wa saa sita mchana. Baadaye, nilielekea katika eneo la Gamba ambako nilifika karibu saa tisa mchana. Hata hivyo tulipokuwa tukikaribia kufika eneo la Nyangoro, umbali wa kilomita 50 kutoka Mokowe, basi letu lilianza kufyatuliwa risasi katika kioo kilicho eneo la dereva. Ikiwa singelisimamisha, abiria wote wangeuliwa,” akasema.

Alisema kuwa baadaye, vijana wanne waliingia katika basi na kusema walikuwa wakiwatafuta watu ambao si Waislamu.

“Nilijawa na wasiwasi. Niliangalia nyuma lakini sikumwona manamba. Walienda kwa kila abiria na kumwambia kusema ombi la Kiislamu liitwalo ‘Shahada.’ Baadaye walikagua kila sehemu ya basi hilo na kuondoka,” akaelezea.

Bw Abdalla alisema kuwa Wakristo waliokuwepo katika basi walifichwa na abiria Waislamu vichwani mwao, huku wengine wakijificha chini ya viti na kujifunika kwa mikoba yao.

Kwenye mashambulio yaliyotokea awali, watu ambao si Waislamu walikuwa wakiuliwa na wapiganaji wa makundi ya kigaidi.

Alisema kuwa jambo jingine lililowaokoa watu hao ni maandishi ya Kiarabu yaliyokuwa yameandikwa kwenye basi hilo, ambapo wahalifu hao waliyafasiri kuwa basi hilo lilimilikiwa na Waislamu.

Alisema wanamgambo hao walisema hawakumpata yule walikuwa wakimtafuta. Alieleza walikuwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 22 na 25.

Mmoja alikuwa akitumia simu kurekodi video huku mwingine akiwa amebeba mkoba mkubwa.“Mmoja alikuja nilikokuwa na kunikumbatia. Alinieleza kwamba tunaweza kuondoka na sipaswi kumweleza yeyote kuhusu yale yaliyotokea,” akasema.

Alieleza kuwa baada yao kusoma maandishi yaliyokuwa yameandikwa kwenye basi hilo, walifasiri kila abiria alikuwa Mwislamu.

Kulingana naye, basi hilo lilipigwa risasi zaidi ya mara nane.“Waliponiambia kuondoka, basi halingeweza kwenda kwani baadhi ya sehemu zake zilikuwa zishaharibika. Hata hivyo, nililizima na kuliwasha tena ambapo nilifanikiwa kuondoka walikokuwa,” akaeleza.

Alisema kuwa wakati gari lilipokataa kwenda, mmoja wa magaidi hao alijaribu kuliendesha japo likakataa.

“Ni kama walikuwa na haraka na muda wao ulikuwa umeisha,” akaeleza.Baada ya kwenda umbali wa karibu kilomita moja, basi hilo lilisimama kwa sababu mafuta yalikuwa yakimwagika.

Kwa bahati nzuri, kulikuwa na dereva mwingine aliyekuwa akimfuata kwa gari aina ya Probox. Alisema hakukutana na magaidi hao. Dereva huyo alikimbia katika Kituo cha Polisi cha Witu kuripoti tukio hilo.

Kulikuwa na ndege aina ya helikopta zilizokuwa zikipaa katika eneo hilo kuwasaka wanamgambo wa kundi la Al Shabaab, waliohofiwa kujificha katika Msitu wa Boni.

Habari zinazohusiana na hii