MMUST, Kabras kualika Quins and Oilers ugani Nandi Bears

Na GEOFFREY ANENE

LIGI Kuu ya raga nchini itarejea katika kaunti ya Nandi kwa mara ya kwanza baada ya miaka nyingi wakati klabu ya gofu ya Nandi Bears itakuwa mwenyeji wa michuano miwili ya ligi hiyo maarufu kama Kenya Cup, mnamo Julai 24.

Timu ya Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) itaalika mabingwa wa zamani Kenya Harlequin kutoka kaunti ya Nairobi saa sita adhuhuri kabla ya wafalme wa 2016 Kabras Sugar kukaribisha Menengai Oilers kutoka kaunti ya Nakuru saa nane mchana. MMUST na Kabras wanatoka kaunti ya Kakamega, lakini watakuwa wakitumia uwanja wa Nandi Bears kama wao wa nyumbani hapo Jumamosi.

Mechi nyingine tatu zimeratibiwa kusakatwa jijini Nairobi.

Uga wa RFUEA kwenye barabara ya Ngong Road utatumiwa kwa michuano miwili ambayo ni Strathmore Leos kutoka mtaani Madaraka dhidi ya mabingwa wa zamani Top Fry Nakuru kutoka Nakuru na washikilizi wa rekodi ya mataji mengi Nondescripts dhidi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta (Blak Blad).

Mabingwa watetezi KCB watakuwa nyumbani katika uwanja wa KCB Ruaraka kuzichapa dhidi ya washindi wa zamani Mwamba. Mashabiki hawaruhusiwi uwanjani katika michuano hiyo yote kwa sababu ya hatari ya virusi vya corona.

Ratiba ya Kenya Cup (Julai 24):

Masinde Muliro vs Kenya Harlequin (12.00pm, Nandi Bears)

Strathmore Leos vs Top Fry Nakuru (1.00pm, RFUEA)

Kabras Sugar vs Menengai Oilers (2.00pm, Nandi Bears)

Nondescripts vs Blak Blad (3.00pm, RFUEA)

KCB vs Mwamba (3.00pm, KCB Ruaraka).