• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Namna ufadhili wa ‘Wings to Fly’ulivyokwamua wanafunzi maskini

Namna ufadhili wa ‘Wings to Fly’ulivyokwamua wanafunzi maskini

Na WINNIE ONYANDO

KWA muda mrefu, maelfu ya watahiniwa wa KCPE ambao walifanya vyema lakini wakakosa karo walitamauka na kupoteza nafasi zao katika shule za kitaifa na za mkoa. Wengi walikuwa mayatima na wale wazazi wao wana mapato ya chini.

Hata hivyo hali hii sasa imebadililka tangu Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya Equity, Dkt James Mwangi azindue mpango wa Wings to Fly mnamo 2010 ambapo watahiniwa kama hao walipata ufadhili wa kuwezesha kukamilisha masomo yao.

Kufikia sasa, watahiniwa zaidi ya 37, 009 wanaotoka katika mitaa mbalimbali nchini wamejiunga na shule za upili.Mwaka huu, jumla ya watahiniwa 10,705 waliofanya mtihani wao wa KCPE, watapokea ufadhili wa masomo chini ya mipango ya Wings to Fly na Elimu Schorlarship.

Kati ya 10,705 watakaonufaika na ufadhili huo, wasomi 1,705 watajiunga na mpango wa Wings to Fly huku wengine 9,000 wakijiunga na mpango wa Elimu scholarship.Mwaka huu, Benki ya Equitly ilipokea maombi zaidi ya 114,765 kutoka kwa watahiniwa mbalimbali nchini ili kujiunga na mipango hiyo mawili.

Benki hiyo hutoa ufadhili wa masomo, kuwanunulia wafadhili vitabu, sare zote, kugharamia nauli ya kumfikisha mwanafunzi shuleni na hata kumpa mwanafuzi pesa za kukidhi mahitaji yake ya kimsingi akiwa shuleni kwa kipindi cha miaka minne.

Katika hafla ya kuwapongeza watahiniwa 1, 283 kutoka kaunti ya Nairobi iliyofanyika Jumanne katika shule ya Upili ya Wasichana ya Pangani, Dkt Mwangi alisema mipango hiyo haifadhili tu elimu kwa watoto bali pia huwapa ushauri na kuwakuza ili wawe viongozi watakaowakuza wengine.

“Elimu ni mchakato wenye nguvu ya mabadiliko. Ukiwafunza vijana, utakuwa umewakuza viongozi wa kuleta mabadiliko kesho,” alisema Dkt Mwangi akiwahutubia watahiniwa. Dkt Mwangi alihimiza ushirikiano wa karibu na serikali kupitia Wizara ya Elimu ili kuwasaidia wanafunzi zaidi hasa wanaoishi na ulemavu na familia ambazo hazijiwezi kifedha.

Mmoja wa walionufaika na mpango wa Wings to Fly mnamo 2016 alimshukuru Dkt Mwangi kwa kumkweza kutoka maisha ya uchochole hadi chuoni.Bi Mariana Wanjiru alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa waliohutubia watahiniwa 1,283 waliobahatika kupata ufadhili kutoka kwa benki ya Equity.

Bi Wanjiru, 20 aliwahimiza watahiniwa hao kutumia nafasi hiyo adimu ipasavyo huku akiwasimulia maisha yake ya awali na jinsi ufadhili huo ulivyompa motisha kutia bidii masomoni ili kuinua familia yake kutoka umaskini mitaani.

“Nilizaliwa na kulelewa mtaani. Mimi na familia yangu tulishinda pipani tukila makombo. Hata nyumba hatukuwa nayo. Nashukuru Dkt Mwangi kwa kuimarisha maisha yangu kielimu,” alisema Bi Wanjiru. Aliwahimiza vijana wanaotoka katika mitaa duni kutozingatia hali yao ya uchochole bali kujiamini na kuwa na moyo wa kuleta mabadiliko katika familia yao.

“Usipotumia nafasi yako vizuri utabaki ukijuta. Dkt Mwangi na wenzake wamejitolea kutusomesha. Usimwaibishe kwa kumletea matokeo mabaya,” aliwasihi watahiniwa.Katika mtihani wake wa kitaifa wa KCSE, binti huyo alizoa alama ya A na kuwa miongoni mwa wanafunzi wachache waliochaguliwa kuendelea na mpango huo hadi Chuo Kikuu.

Dkt Mwangi pamoja na kundi lake waliahidi kumpa mwongozo na kuhakikisha ametimiza ndoto yake. “Tutakaa naye karibu na kumpa mwongozo unaofaa. Ikiwezekana atapata ufadhili wa kusomea ng’ambo,”alisema Dkt Mwangi.

Benki hiyo ikishirikiana na Mastercard Foundation, Serikali ya Ujerumani kupitia KfW, Benki ya Dunia (SEQIP), serikali ya Kenya pamoja na wadhamini wengine wamekuwa wakichanga pesa za kutosha ya kuwafadhili wanafunzi kama hao.

Kamati za uteuzi zinajumuisha wanachama kati ya kumi na moja na kumi na tatu na zinaongozwa na Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti Ndogo kwa msaada na uratibu kutoka kwa matawi mbalimbali ya benki hiyo.

Wao hufanya uteuzi kupitia njia ya mahojiano wa moja kwa moja na wazazi au walezi wa watahiniwa na baadaye kuwatembelea nyumbani ili kuthibitisha hali yao halisi.Mwaka huu, Dkt Mwangi alitoa msaada wa sola, redio, taa na betri kwa familia ambazo hazina nguvu za umeme ili kuwasaidia katika masomo yanayotolewa na KICD inayoenda sambamba na masomo yao.

Mtahiniwa ambaye atapata alama ya A katika mtihani wa kitaifa ya KCPE hupewa ufadhili wa Sh4,000 kwa wasichana na Sh3,500 kwa wavulana kuhakikisha wanamudu mahitaji na kuwaweka mbali na uovu wa kijamii.

Dkt Mwangi aliwahimiza watahiniwa watie bidii katika masomo yao ili kuwaondoa wazazi wao katika maisha duni.w

  • Tags

You can share this post!

Vyombo vya habari vishirikiane na NLC kuripoti visa vya...

Sheria Mpya: Madume yalitapeli wanawake!