Sheria Mpya: Madume yalitapeli wanawake!

Na DOUGLAS MUTUA

AKUFUKUZAYE hakwambii ‘toka’. Hiyo ndiyo kauli ya wahenga ambayo inapaswa kutiliwa maanani zaidi na vimada, almaarufu ‘slayqueens’, wanaotafuna pesa za matajiri.

Nasema ‘matajiri’ kwa sababu mkono mtupu tangu hapo haulambwi, na tunaelewa walio nazo tele benki si wengi mno, hasa nyakati hizi za janga la corona.Juzi Bunge limepitisha sheria inayosema kwamba mwanamke na mwanamume wanaoishi pamoja bila kufunga ndoa rasmi hawawezi kurithi mali iwapo mmoja kati yao ataaga dunia.

Sheria hiyo inakinzana na Katiba, inayotambua wazi kuwa mwanamke na mwanamume wakiishi pamoja kwa miaka mitatu wanatambuliwa kuwa mke na mume.Iwapo mtu hatakimbia mahakamani kulalamika kwamba sheria hiyo mpya inawapa waliotawaliwa na taasubi ya kiume mshawasha wa kukiuka Katiba, basi itatumika ilivyo.

Na hapo ndipo ambapo vimada walio radhi kuishi kisiri na matajiri wakisubiri miaka mitatu itimie ili wajitangaze wake zao watakapopata taabu sana.Nasisitiza kuwa vimada hao wanapaswa kutafakari sana kuhusu mustakabali wa mahusiano ya aina hiyo kwa sababu wanaume waliopitisha sheria hiyo hawakuwajali.

Madume walipania kukinga mali yao dhidi ya wapenzi wao. Walisema wapenzi wa siri wana mazoea ya kujitokeza na kuwashtaki wajane ili nao wagawiwe mali mara tu mwanamume tajiri anapofariki.Kuna mambo matatu ya kupendeza kuhusu mtazamo wa wabunge wa kiume ambao walipitisha sheria hiyo kinyume na mapenzi ya wenzao wa kike.

Kwanza, walizungumza kana kwamba wana hakika ya aslimia 100 kuwa wanaume walio na vimada ndio watakaofariki kabla ya vimada wao. Kuishi au kufa ni milki ya Mungu.Pili, walizungumza kana kwamba ni wanaume pekee waliojaaliwa nafasi ya hali katika jamii, hivi kwamba ndio tu wanaokuwa wahanga wa kutafuniwa mali wakifariki.

Si siri kwamba kuna wanawake matajiri na jasiri, ambao hawapepesi macho wanapowatongoza wanaume na kuwaweka rumenya. Mwanamke tajiri akifariki je?Tatu, walimsawiri mwanawake kama kiumbe dhaifu, mlafi na mjanja anyemeleaye mali kama fisi anavyomfuata mtu akidhani mkono ni mnofu unaoweza kuanguka akala nyama.

Tunajua kuna wanaume – hasa vijana wa siku hizi ambao ni wavivu kupindukia – wanaolaza damu na kusubiri kutunzwa na wanawake wenye mafedha ya kumwaga.Kimsingi, kwamba Bunge lilipitisha sheria hiyo ni ithibati tosha kuwa wanaume wa Kenya wamekataa kubadilika – wanawatizama wanawake kama kupe wafyonza damu.

Kwa hivyo, kutokana na ubinafsi wao wa kupindukia, wamejipa fursa ya kipekee ya kuchovya asali bila majukumu ya kulitunza buyu au kuuchonga mzinga.Ikiwa Katiba inatambua mwanamke na mwanamume wakiishi pamoja kwa miaka mitatu ni wanandoa halali, manufaa ya ndoa yenyewe ni yepi ilhali sheria hiyo mpya imeyatwaa?

Wanaume walio na fikra kama hizo wanataka kuendelea kutumia wasichana wa watu kama shashi ambayo hutupwa bila shukrani kwenye chumba cha mtu yeyote mstaarabu.Kwa kuwa wanaume matajiri hawadhani wanaume maskini ni watu, hawajali wala kubali ni yepi yatakayowakumba iwapo wake zao wa miaka mitatu, tena matajiri, wataaga ghafla.

Ajabu ni kwamba, kwa kuwa Kenya ni taifa la kibebari linalozingatia sera za uchumi huru, wanaume na ubabe wote huo hawatakosa vimada wa kutumia na kutupa.

Kisa na maana? Wasiotahadhari wana mji wao; watu wanaotafuta mahusiano kwa madhumuni ya kunufaika kifedha bila kujali kitu kingine chochote hawakosekani.Mmoja akishupaza shingo na kudai ana heshima zake, wa pili ataiona hiyo kama fursa na kuitwaa mara moja!Wanataka pesa za haraka wajiendee zao.

Hiyo ndiyo hali ya mahusiano nchini Kenya. Umalaya, biashara isiyohitaji mtaji, umebatizwa majina yanayotamkika vizuri.Ujuaji unaoitwa usasa haupaswi kuthaminiwa kuliko ukale wenye tija.