Ajowi, Akinyi wafuzu kwa raundi 2 bila jasho Tokyo

Na CHARLES ONGADI

HATIMAYE ratiba ya michuano ya ndondi katika Michezo ya Olimpiki imetolewa huku mabondia wawili wa timu ya taifa Hit Squad, tayari wakifuzu kwa raundi ya pili.

Mshindi wa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Africa Zone 3 Championship nchini DRC Elly Ajowi na Elizabeth ‘ Black Current ‘ Akinyi wamefuzu hadi raundi ya pili bila jasho.Ajowi anayezichapa katika uzito wa heavy, ameratibiwa kupepetana na Cruiz Julio wa Cuba katika mzunguko wa pili siku ya jumanne (Julai27,2021).

Siku hiyo ya jumanne, Akinyi atakutana na Panguana Alcinda Helena wa Msumbiji kwa mara nyengine baada ya kukutana katika mashindano ya Africa Zone 3 Championship nchini DRC.

Akizungmzia pigano lake, Akinyi amesema amejiandaa vya kutosha na kurekebisha makosa yaliyojiri walipokutana nchini DRC na ana uhakika wa kung’oka na ushindi katika pigano la uzto wa welter.

Aidha , leo (jumamosi) nahodha Nick ‘ Commander ‘ Okoth atakuwa wa kwanza ulingoni kuzichapa dhidi ya Erdenebat Tsendbaatar wa Mongolia katika pigano la uzito wa unyoya.Okoth amesema kwamba wala hatishwi na yeyote kutokana na mazoezi makali ambayo amepata kwa kipindi cha miaka miwili chini ya wakufunzi wake wenye tajriba.

“Nitaonesha uwezo wangu leo na wala sina hofu na lolote lile,” akasema nahodha huyu anayeshiriki Michezo ya Olimpiki kwa mara ya pili.Siku ya jumapili itakuwa ni zamu ya Christine Ongare kumaliza udhia dhidi ya Magno Irish wa Ufilipino katika pigano la fly.

Ongare amekiri kwamba hana habari na mpinzani wake lakini atapata kumfahamu barabara watakapokabiliana jukwaani huku akiwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi.

Akizungumza na wanahabari kutoka Tokyo nchini Japan, kocha mkuu Musa Benjamin amekiri kwamba droo iliyofanywa itakutanisha mabondia wake na mibabe ya ngumi duniani.

‘Ili kuwa bingwa ni lazima umshinde bingwa hivyo sina wasiwasi wala hofu kwa mabondia wangu kwa sababu naamini wana kila uwezo wa kushinda mapigano yao,” akasema kocha Benjamin.