• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Mahakama iko msalabani sasa,alalama Koome

Mahakama iko msalabani sasa,alalama Koome

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI Mkuu Martha Koome amesema kuwa majaji wamekumbwa na hofu kufuatia kunaswa kwa wenzao wawili Alhamisi na maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) kwa madai ya kuchukua hongo ya Sh5 milioni.

Chama cha Mahakimu na Majaji nchini (KMJA) jana kiliwasilisha kesi mahakamani kupinga kushtakiwa kwa majaji Aggrey Muchelule na Said Juma Chitembwe.

Akikashfu kukamatwa kwa majaji Muchelule na Chitembwe, Jaji Koome alisema “kama mkuu wa idara ya mahakama na mwenyekiti wa tume ya huduma za mahakama (JSC), hakujulishwa na DCI kama majaji hao walikamatwa”.

“Sikujulishwa na DCI kama anawachunguza majaji hao wawili,” alisema Jaji Koome, akiongeza, “Na wala sikufahamishwa watakamatwa.”Hata hivyo, Jaji Koome alisema katika taarifa kwa wanahabari kwamba amekutana na majaji hao wawili na wakamweleza kilichotokea Alhamisi.

Jaji Koome alisema majaji hao walimweleza jinsi maafisa wa idara ya uchunguzi wa jinai walivyowavamia katika afisi zao katika Mahakama Kuu Milimani na kupekuapekua afisi zao lakini hawakupata pesa zozote za hongo walizokuwa wamepokea.

Licha ya kukiri kutiwa nguvuni kwa majaji Muchelule na Chitembwe kumezua kiwewe na taharuki katika idaara ya mahakama, Jaji Koome aliwahakikishia majaji wako salama na kazi yao imelindwa na Katiba.“Msihofu, muendelee kutekeleza kazi zenu bila woga.

Haki zenu na kazi yenu imelindwa na Katiba,” Jaji Koome aliwaeleza majaji wote katika idara ya mahakama.Jaji Koome aliye pia Rais wa Mahakama ya Juu na mwenyekiti wa JSC alisema majaji hao walihojiwa na kuandikisha taarifa kisha wakaruhusiwa kwenda nyumbani.

Mkurugenzi wa DCI, George Kinoti alikiri katika ujumbe aliotuma kwa mtandao wake akisema majaji hao walikamatwa na kuandika taarifa kisha wakaachiliwa.Katika kesi ya KMJA, mawakili Danstan Omari , Cliff Ombeta na Shadrack Wamboi walisema kukamatwa kwa majaji hao wawili kumezua hali ya taharuki miongoni mwa majaji wote.

“Nani yuko salama ikiwa majaji ambao hutunza katiba ya nchi hii wanakamatwa kiholela pasi sababu yoyote maalum,” alisema Bw Omari. Bw Ombeta alieleza mahakama kuwa sheria na haki za majaji hao wawili zimekandamizwa na maafisa hao waliowakamata bila sababu na bila kibali cha korti kilichowawezesha kuwahoji na kupekua afisi zao.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji alijitenga na kukamatwa kwa Majaji Muchelule na Chitembwe akisema, “Sikujua sababu zilizopelekea wawili hao kukamatwa na kuhojiwa.

”Katika kile kinachoonekana kuwa tofauti kati ya DPP na DCI katika utenda kazi , Bw Haji alisema afisi yake haijapokea faili za majaji hao wawili za madai ya ufisadi. Katika taarifa, Bw Haji alikanusha kutoa maagizo majaji hao watiwe nguvuni.

Akikanusha madai ya chama cha wanasheria nchini (LSK) kikimlaumu Haji kwa kukamatwa kwa majaji hao, kinara huyo wa afisi ya DPP alisema hajapokea faili kutoka kwa afisi ya DCI akiomba ushauri.

“Katika kesi ya KMJA, mahakama kuu inaombwa ifutilie mbali hatua ya kuwafungulia mashtaka wawili hao kwa kuwa JSC haikufahamishwa chochote na DCI kuwahusu wawili hao iwachukulie hatua,” Mabw Omari, Ombeta na Wambui walisema na kuongeza, majaji watano waliosikiza kesi ya kupinga kushtakiwa kwa Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu walisema “lazima JSC ijulishwe kabla ya jaji yeyote kukamatwa”.

KMJA inaomba mahakama kuu ikashfu kitendo hicho cha kuwadhulumu na kuwakejeli majaji hao.

  • Tags

You can share this post!

Corona: Uhaba wa vifaa vya upimaji nchini

Uhuru akutana na magavana 5 kupanga ziara magharibi