Uhuru akutana na magavana 5 kupanga ziara magharibi

Na DERICK LUVEGA

MAGAVANA watano kutoka eneo la Magharibi mnamo Alhamisi walikutana na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kiongozi wa nchi kufanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo eneo hilo mwezi ujao.

Magavana hao tayari wameorodhesha miradi kadha ambayo Rais Kenyatta atazindua katika ziara hiyo inayojiri miezi miwili baada yake kuzuru na kuzindua miradi katika eneo la Luo Nyanza.

Baada ya ziara hiyo ambapo Rais pia aliongoza Sherehe za Madaraka Dei jijini Kisumu, viongozi wa Magharibi walilalamika kuwa Rais Kenyatta ametenga eneo hilo kimaendeleo.

Wakiongozwa na seneta wa Kakamega Cleophas Malala, wanasiasa hao walidai eneo la Luo Nyanza limevuna pakubwa kimaendeleo tangu aliporidhiana kisiasa na kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Machi 9, 2018.Walidai eneo la Magharibi limetengwa licha ya kwamba wakazi wamekuwa wakimuunga mkono Bw Odinga katika chaguzi kadha zilizopita.

Mnamo Alhamisi, Rais Kenyatta alikutana katika Ikulu ya Mombasa na magavana; Wycliffe Oparanya (Kakamega), Sospeter Ojaamong (Busia), Patrick Khaemba (Trans Nzoia), Dkt Wilbur Otichillo (Vihiga) na Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati.

Ziara hiyo ya Rais Kenyatta eneo la Magharibi inasubiriwa kwa hamu na ghamu na wakazi wa eneo hilo japo limegawanyika kisiasa.

Baadhi ya wanasiasa wanaegemea mrengo wa kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula kwa upande mmoja huku wengine kama vile Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli na Gavana Oparanya wakiegemea mrengo hasimu ambao ni wandani wa kiongozi wa ODM Raila Odinga.