Kamishna apiga marufuku wakazi kula matangani

Na BRIAN OJAMAA

KAMSHNA wa Kaunti ya Bungoma, Bw Samuel Kimiti, amepiga marufuku kula kwa matanga akisema agizo hili linanuia kupunguza msambao wa virusi vya corona.

Akizungumza na wanahabari ofisini mwake mjini Bungoma, Bw Kimiti alionya kuwa mazishi yataruhusiwa tu kufanyika kwa muda wa saa 72 kama ilivyoamrishwa na serikali.Vilevile, waombolezaji ni 50 pekee kujumuisha jamaa na marafiki wa karibu wa mwendazake.

“Tumepata kuwa nyakati za mlo na densi matangani watu wanatangamana mno, na hilo limechangia ongezeko la maambukizi ya corona nchini,” alieleza.Pia alionya yeyote atakayepatikana nje kuanzia saa moja jioni atakamatwa, ikiwemo waendeshaji bodaboda.

Wanaofanya kazi masaa ya kafyu kuwa watakamatwa na kushukiwa kuwa wezi.Alionya watu kuuchukulia ugonjwa huo tahadhari kwa kuwa wengi wamepoteza wapendwa wao kupitia virusi hivyo.

“Msipuuze ugonjwa huu kwa kuwa wengi wamepoteza wapendwa wao hasa kwa kutojali,” alionya.Alisema pia kuwa watakaohudhuria mazishi na kuleta fujo hasa wanasiasa wanaoleta machafuko kwenye matanga watachukuliwa hatua.

“Ni jambo la kusikitisha ikiwa familia imepoteza mpendwa wao na wengine kuhudhuria mazishi nia yao ikiwa ni kuleta fujo ikiwemo wanasiasa,” alisema kamishna huyo.Kadhalika, alisema kuwa polisi watahudhuria mazishi ili kuhakikisha kuwa Amani imedumishwa na watu kufuata kanuni za serikali za kudhibiti msambao wa corona.

Bw Kimiti aliwaomba wakaazi hao kushirikiana na serikali kwa kuzingatia kanuni zilizotolewa kama vile, kuosha mikono kila mara, kuvaa barakoa na kutokaribiana ili kupambana na janga hilo.Aliwaonya polisi ambao wanachukua hongo kutoka kwa wamiliki baa na kuwaruhusu kufanya kazi wakati wa kafyu kuwa watachukuliwa hatua.

“Watakao patikana wakifanya kazi wakati wa kafyu watakamatwa. Polisi ambao wanachukua hongo kutoka kwa wamiliki baa watakamatwa na kujibu mashaka mbele ya korti,” alisema.Yeyote atakayepatikana nje kuanzia saa moja jioni atakamatwa.

Aliwaonya waendeshaji bodaboda wanaofanya kazi masaa ya kafyu kuwa watakamatwa na kushukiwa kuwa wezi.Katika siku mbili zilizopita, polisi wamewakamata waendeshaji bodaboda pamoja na wamiliki baa wengi waliovunja kanuni za kafyu.

“Wengi wamekamatwa kwa kupatikana nje hasa masaa ya kafyu. Kila mmoja ahakikishe kuwa amefika kwake kabla ya saa moja usiku,” alisema Bw Kimiti.