• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Masaibu yalivyomwandama Jaji Muchelule kwa miaka 14

Masaibu yalivyomwandama Jaji Muchelule kwa miaka 14

Na RICHARD MUNGUTI

JAJI wa Mahakama Kuu, Aggrey Muchelule amekuwa akikumbwa na masaibu tele kwa zaidi ya miaka 14 iliyopita.Jaji Muchelule amekuwa akikumbana na vizingiti chungu nzima kutoka kwa serikali.

Mbali na kutoapishwa mwezi uliopita kuwa Jaji katika Mahakama ya Rufaa, sasa Jaji Muchelule amejikuta katika dhiki ya kuchunguzwa na maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) kwa madai ya kushiriki ufisadi.

Alhamisi, maafisa wa polisi kutoka kitengo cha DCI walimvamia jaji huyo katika afisi yake kisha wakamtia nguvuni ili kumhoji.

Masaibu ya Jaji Muchelule yalianza mnamo 2006 wakati Rais Mstaafu Mwai Kibaki alipokataa kumteua pamoja na majaji wengine wawili. Hii sasa ni mara ya pili tangu 2006 mwanasheria huyo kujikuta katika hali ya sintofahamu.

Jaji Muchelule pamoja na majaji wengine 40 waliteuliwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kujiunga na Mahakama ya Rufaa.

Lakini Rais Kenyatta alikataa jina lake pamoja na majaji wengine watano akidai palikuwa na madai ya ufisadi.Mnamo Desemba 2006, Jaji Muchelule alikuwa anahudumu kama hakimu mkuu katika mahakama ya Nairobi alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Pamoja na aliyekuwa hakimu mkuu katika mahakama ya Eldoret wakati huo Bi Florence Muchemi, waliteuliwa kuwa majaji katika mahakama kuu.

Wakati huo huo, vilevile, tume ya JSC ilimteua Jaji Ali Abida Aroni kuwa jaji katika mahakama ya kuamua kesi za mizozo ya wafanyakazi na waajiri (ELRC).

Watatu hao; Jaji Muchelule, Jaji Muchemi na Jaji Aroni walijivika mavazi rasmi kisha wakafululiza hadi Ikulu ya Nairobi kula kiapo.Wakisubiri aliyekuwa Bw Kibaki, ghafla hafla hiyo yao ya kiapo alifutiliwa mbali.Bw Kibaki hakuwaapisha majaji Muchelule, Aroni na Muchemi.

Katika muda wa miezi miwili Bw Muchelule alihamishwa kutoka mahakama ya Nairobi na kupelekwa mahakama ya Embu naye Bi Muchemi akapelekwa Naivasha kama hakimu mkuu.

Baada ya miaka mitatu 2009 Jaji Muchelule aliteuliwa kirasmi kuwa Jaji mahakama kuu.Rais Kenyatta alikataa kumteua Jaji Muchelule , Jaji Weldon Korir, Jaji George Odunga,Jaji Prof Joel Ngugi na Bi Judith Omange na hakimu mkuu Evans Makori.

Masuala kadhaa yamezuka dhidi ya Jaji Muchelule wakati wa utenda kazi wake hasa alipowaachilia huru aliyekuwa kinara wa ulanguzi wa dawa za kulevya marehemu Ibrahim Akasha 2005 na mwanawe Baktash Akasha anayetumikia kifungo cha gerezani cha miaka 25 nchini Amerika.

Ibrahim na Baktash walikabiliwa na shtaka la ulanguzi wa mihandarati.Watoto wa Akasha aliyeuliwa Netherlands walikamatwa na kusafirishwa hadi Amerika na maafisa wa ujasusi wa Amerika kwa tuhuma za ulanguzi wa mihandarati.

Baada ya kushikwa watoto hao wa Akasha walikiri kushiriki katika visa vya ulanguzi wa mihandarati.Jaji Muchelule na Jaji Said Juma Chitembwe walikamatwa kwa madai ya ufisadi wa Sh5 milioni.

Baada ya kuhojiwa waliachiliwa lakini Mahakama kuu imetoa agizo wawili hao wasikamatwe na kufunguliwa mashtaka hadi kesi iliyowasilishwa na chama cha mahakimu na majaji KMJA isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Muchelule ndiye mkuu wa kitengo cha kesi za kifamilia na urithi katika mahakama kuu.Jaji Chitembwe alikamatwa miaka 12 iliyopita na kushtakiwa pamoja na mawakili Edward Muriu Kamau na Stephen Kipkenda Kiplagat kwa kuhusika na uuzaji wa ardhi ya NSSF ya thamani ya Sh1.3bilioni.

Lakini watatu hao waliachiliwa na Jaji Chitembwe kuendelea na kazi.Jaji Chitembwe alikuwa mmoja wa waliowania wadhifa wa Jaji Mkuu na Jaji wa Mahakama ya Juu.

You can share this post!

JAMVI: Huenda miswada isaidie Uhuru, Raila kuandaa refarenda

Mabilioni ya miradi ya serikali ndiyo ‘hutafunwa’ zaidi...