• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
KDF yaungana na GSU, Kenya Prisons na KPA fainali za voliboli

KDF yaungana na GSU, Kenya Prisons na KPA fainali za voliboli

Na AGNES MAKHANDIA

WANAJESHI wa KDF wamejikatia tiketi ya kushiriki mechi za muondoano za timu nne-bora za Ligi Kuu ya voliboli ya wanaume baada ya kushinda mechi zake mbili za mwisho za msimu wa kawaida ugani Nyayo, Jumapili.

KDF walipepeta Nairobi Prisons kwa seti 3-0 za alama 25-18, 25-17, 25-18 kabla ya kukamilisha msimu wa kawaida kwa kuzaba Polisi wa Utawala 3-0 (25-18, 25-21, 27-25).

Wanajeshi hao, ambao wanatiwa makali na Elisha Aliwa, sasa wanajiunga na mabingwa watetezi GSU pamoja na washindi wa zamani Kenya Prisons na timu ya Halmashauri za Bandari Kenya (KPA) waliofuzu mapema.

Katika mahojiano, Aliwa alikiri kuwa walijinyanyua msimu ukielekea kutamatika, lakini amefurahia kunyakua tiketi ya mwisho.

“Presha ilikuwepo. Tulifahamu fika kuwa timu ya Shirika la Huduma ya Misitu (KFS) na wanabenki wa Equity pia wanawinda tiketi hiyo moja iliyokuwa imesalia. Nafurahia kuwa tumepata tiketi siku ya mwisho, ingawa kazi ya kutafuta mafanikio zaidi ndiyo inaanza,” alisema Aliwa.

“Baada ya kutazama michuano ya wikendi, hasa ile iliyokutanisha GSU na KPA, nimepata picha kuwa mechi za muondoano hazitakuwa rahisi. Tutahitaji kuwa imara zaidi ili kupigania taji,” alisema.

Mchuano kati ya GSU na KPA ulishuhudia GSU ikitoka chini seti moja na kushinda 3-1 (25-15, 26-28, 20-25, 13-25) na kukamilisha msimu bila kushindwa.

Nahodha wa GSU, Shadrack Misiko alisema kuwa wanafurahia sana kumaliza msimu wa kawaida bila kupoteza mechi.

“Lengo letu sasa ni kutetea taji letu. Mashindano yatakuwa makali, lakini naamini kuwa tuna uwezo,” alisema mzuiaji huyo wa kati.

Mshambuliaji Abiud Chirchir alisaidia GSU kujinyanyua katika mchuano huo baada ya kuanza kutumiwa mwisho wa seti ya kwanza.

Chirchir alijaza nafasi ya Kelvin Omuse ambaye alijiunga na GSU kutoka Equity mwaka 2020.

Makombora ya kuanzisha mechi yalisaidia KPA kung’ara katika seti ya kwanza.

Hata hivyo, GSU iliimarisha mashambulizi na pia uzuiaji wake wa makombora ya karibu na wavu ikitawala seti tatu zilizofuata.

Equity pia ilitoka chini seti moja ikichabanga KFS 3-1 (24-26, 25-19, 25-23, 25-19).

Mshindi wa ligi pamoja na nambari mbili watafuzu kushiriki makala yajayo ya mashindano ya klabu za Afrika.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

DINI: Unayojiambia yatakuinua au kukufifisha, tafakari...

Hafnaoui ashindia Tunisia dhahabu ya uogeleaji kwenye...