• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Washirika wa Kalonzo wapuuza hatua ya Kibwana

Washirika wa Kalonzo wapuuza hatua ya Kibwana

Na PIUS MAUNDU

BAADHI ya washirika wa kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, wamepuuzilia mbali hatua ya baadhi ya wazee kutoka Ukambani kumuunga mkono Gavana Kivutha Kibwana wa Makueni kuwania urais 2022.

Prof Kibwana aliungwa mkono huo kutoka kwa Baraza la Koo za Jamii ya Akamba (ACGC), lililomtembelea kumjulia hali baada ya kuugua. Baraza hilo linawakilisha koo zote 22 za jamii hiyo.

“Tunaunga mkono azma yako kuwania urais,” akasema Bw Boniface Kilonzo, ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza hilo.

Baraza hilo lilitoa msimamo huo Ijumaa, katika mji wa Wote. Kauli ya Bw Kilonzo pia iliungwa mkono na katibu mkuu wa baraza hilo, Bw Davis Maeke.

Wazee hao walimsifu Prof Kibwana kama kiongozi shupavu, anayejali na kupigania maslahi ya jamii ya Akamba.

Walisema kuwa gavana huyo ana uwezo mkubwa kuiongoza jamii na nchi nzima kwa jumla kupata ufanisi katika sekta zote.

Ikizingatiwa Bw Musyoka na Gavana Alfred Mutua wa Machakos pia wametangaza azma ya kuwania urais, wazee hao walimtaka Prof Kibwana kuwaunganisha viongozi wote wa kisiasa kutoka eneo hilo.

Walisema anapaswa kuiongoza jamii kwa mazungumzo ya kubuni miungano ya kisiasa na maeneo mengine “ili kuiwezesha kuwa sehemu ya serikali ijayo”. Eneo hilo lina karibu wapigakura 1.5 milioni.

Hata hivyo, Seneta Mutula Kilonzo Junior (Makueni) na mbunge Daniel Maanzo (Makueni) walipuuzilia mbali hatua hiyo, wakiitaja kama hafifu na isiyokuwa tishio kwa siasa za Bw Musyoka.

“Viongozi hao walipaswa kuomba ushauri kwa wenzao kabla ya kutangaza kumuunga mkono Prof Kibwana. Wanapaswa kukataa kutumiwa na viongozi kuendeleza maslahi yao ya kisiasa,” akasema Bw Maanzo.

You can share this post!

Japan wapepeta Mexico na kuendeleza ubabe wao kwenye...

Uchaguzi: Mrengo wa Ruto watishia kushtaki Kenya UN