• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Uchaguzi: Mrengo wa Ruto watishia kushtaki Kenya UN

Uchaguzi: Mrengo wa Ruto watishia kushtaki Kenya UN

Na WAANDISHI WETU

MJADALA kuhusu tarehe ya Uchaguzi Mkuu 2022 umeibua cheche za maneno, huku wanasiasa wanaomuegemea Naibu Rais William Ruto wakitishia kuishtaki serikali kwa Umoja wa Mataifa (UN).

Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali, na aliyekuwa Seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, walisema Chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho Dkt Ruto anatarajia kutumia kuwania urais 2022, hakitakubali uchaguzi uahirishwe.

“Tutapinga hilo na hata kuandika barua kwa Baraza la Usalama katika Umoja wa Mataifa (UN) kueleza kuwa Kenya haiko vitani, na hivyo serikali inafaa kuweka mipango ya kuhakikisha uchaguzi utafanyika jinsi ilivyopangwa,” akasema Bw Omar.

Wiki iliyopita, Mahakama ya Afrika ilichapisha maoni kwa mataifa ya Afrika ambayo hayatakuwa na uwezo wa kuandaa uchaguzi kwa sababu ya janga la corona, yazingatie kuahirisha; japo ikiwa tu kuna sheria za kitaifa zinazoruhusu uahirishaji wa Uchaguzi Mkuu.

Katiba inahitaji Uchaguzi Mkuu kufanyika mwaka wa tano baada ya kila uchaguzi, katika Jumanne ya pili ya mwezi Agosti.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) tayari ilitangaza uchaguzi utafanyika Agosti 9, 2022.

“Janga kuu zaidi litakuwa kuendelea kuishi chini ya serikali hii iliyojaa ubaguzi katika utoaji huduma kwa Wakenya.

“Hatutakaa kitako tukitazama uchaguzi uahirishwe kinyume cha Katiba. Wale wanaoshinikiza hilo wanajua wamepoteza umaarufu mashinani na sasa wanataka muda zaidi wajiandae kwa uchaguzi,” alisisitiza Bw Omar.

Naye Bw Ali aliongeza: “Kuna viongozi wa kaunti na wengine katika serikali kuu ambao wamekuwa wakijaribu kuninyamazisha. Sitanyamaza wakati watu wachache wanata kunufaika huku wananchi wakiteseka.”

Wawili hao walikuwa wakizungumza katika kikao cha wanahabari mjini Mombasa, baada ya kuzindua upya shughuli ya kusajili wanachama katika UDA.

Akizungumza katika eneo la Ruriri, Kaunti ya Nyandarua, Mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro alisema hawatakubali tarehe hiyo ibadilishwe.

“Ushauri uliotolewa na Mahakama ya Afrika haujaipa Kenya kibali cha kuahirisha uchaguzi. Sisi tarehe yetu inalindwa na Katiba,” akasema mbunge huyo katika hafla ambapo Dkt Ruto alikuwa ameenda kuwashukuru wakazi kwa kuchagua MCA wa chama cha UDA.

Gavana wa Pokot Magharibi Prof John Lonyangapuo alionya kuwa uvumi kuhusu njama ya kuairisha uchaguzi mkuu unaweza kutumbukiza taifa katika machafuko. Alisema siasa za aina hiyo ni hatari kwa nchi.

“Tunafaa kukomesha uvumi na propaganda kuhusu suala hilo. Hata kama ni ukweli, wacha ije. Tupunguze joto la kisiasa na kuhudumia Wakenya,” akasema Prof Lonyangapuo mjini Kanyarkwat alipokagua miradi.

Naye kinara wa Narc Kenya, Bi Martha Karua, akizungumza Jumamosi katika kijiji cha Riandira, Kaunti ya Kirinyaga, alisema tarehe ya chaguzi inaweza tu kubadilishwa iwapo Kenya iko katika vita na taifa lingine.

“Kwa sasa, Kenya ina amani; tarehe ya chaguzi inapaswa kusalia ilivyo,” waziri huyo wa zamani wa masuala ya Katiba alieleza na kuwataka Wakenya kusimama kidete kukataa njama zozote za kuahirishwa kwa uchaguzi.

“Tunafaa kujiandaa kukataa njama zozote za serikali kuahirisha tarehe ya uchaguzi. Ni sharti kura ifanyike kuambatana na Katiba,” alisema.

Ripoti za ANTHONY KITIMO, JOSEPH OPENDA, MARY WANGARI, OSCAR KAKAI na GEORGE MUNENE

You can share this post!

Washirika wa Kalonzo wapuuza hatua ya Kibwana

Utalii wapigwa jeki Lufthansa ikizindua safari