• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
Wanawake saba wakamatwa kwa kutengeneza pombe haramu kwenye mtaa wa mabanda

Wanawake saba wakamatwa kwa kutengeneza pombe haramu kwenye mtaa wa mabanda

Na SAMMY KIMATU

WANAWAKE saba walikamatwa mnamo wikendi kwa madai ya kuendesha biashara ya kutengeneza pombe haramu katika mtaa mmoja wa mabanda.

Aidha, zaidi ya lita 100,000 za pombe aina ya Kangara zilinaswa na kuharibiwa.

Operesheni hiyo iliendeshwa na maafisa wa polisi wa kutoka kituo cha Industrial Area na kile cha Reuben.

Msako huo ulifanyika katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kwa Reuben ulioko katika kaunti ndogo ya Embakasi Kusini.

Mkuu wa polisi katika eneo la Makadara, Bw Timon Odingo aliambia Taifa Leo kwamba wateja wa washukiwa walifanikiwa kukwepa mtego wa polisi.

Wakati wa msako huo, kulikuwa na sinema ya bwerere baada ya wakazi kusitisha shughuli zao za kila siku ili washuhudie matukio.

Bw Odingo aliongeza kwamba washukiwa sugu hao walikuwa wakiendesha kiwanda cha kutengeneza chang’aa katika mtaa huo kwa muda mrefu.

Isitoshe, wateja walikuwa wakinunua pombe hiyo kwa bei ya jumla kisha nao wakienda kusambazia wauzaji wa rejareja katika mitaa mingine Kaunti ya Nairobi.

“Kilikuwa ni kiwanda cha kutengeneza chang’aa kwa muda mrefu huku kukiwa na mchezo wa paka na panya kati yao na maafisa wetu kila wakati operesheni ikipangwa. Hata hivyo, siku zao arobanne zimetimia,” Bw Odingo akanena.

Kwa mujibu wa ripoti za ujasusi, wauzaji wa pombe haramu wamechangia pakubwa utovu wa usalama katika maeneo mengi kaunti ya Nairobi huku vijana wakizama kwa uraibu wa ulevi.

Vile vile, Bw Odingo alifichua kwamba baadhi ya nyumba za kuuzia pombe haramu hutumiwa pia kama maficho ya wahalifu.

Kadhalika, aliongeza kwamba vijana wengi wamezembea na kulegeza kamba katika kuchapa kazi kwa minajili ya ujenzi wa taifa.

Isitoshe, baadhi ya wanaume wameshindwa na shughuli za kuwajibikia ndoa zao nyumbani huku wake zao wakitumia mashirika mbalimbali kulalamika kuhusu ndoa zao kusambaratika.

Mapema mwaka 2020, msako mwingine sawa na huo uliendeshwa na aliyekuwa mkuu wa tarafa ya South B, Bw Barre Ahmed katika mitaa ya mabanda ikiwemo Kayaba, Hazina, Fuata Nyayo, Mariguini na Commercial.

“Wakati huo tulikamata washukiwa zaidi ya kumi na kuharibu aina mbalimbali ya pombe haramu isiyopungua lita zaidi ya 50,000,” Mwenyekiti wa usalama katika mtaa wa mabanda wa Kayaba, Bw Jacob Ibrahim akasema.

Kwingineko, maafisa wa utawala walifanya msako mkali ambao haujawahi kufanyika katika kaunti ndogo ya Makadara miaka kadhaa iliyopita.

“Operesheni zilizofanywa na aliyekuwa mkuu wa tarafa ya Makadara, Bi Margaret Mbugua na aliyekuwa kamanda wa polisi katika kambi ya Lunga Lunga, Inspekta Alphonce Nzova Mulinge zimekuwa kumbukumbu katika rekodi za serikali hadi wawili hao wakapandishwa vyeo vyao,” mdokezi kutoka kitengo cha polisi akaambia wanahabari.

You can share this post!

Ufaransa wazima ndoto ya Afrika Kusini kwenye Olimpiki

Rhonex Kipruto kuwa kizibo cha nyota Geoffrey Kamworor mbio...