• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Familia yaahirisha mazishi ya Kangogo

Familia yaahirisha mazishi ya Kangogo

BARNABAS BII na ONYANGO K’ONYANGO

FAMILIA ya konstebo Caroline Kangogo imesimamisha mipango ya mazishi yake, ikisubiri matokeo ya upasuaji wa maiti hiyo.

Mazishi hayo yalikuwa yamepangwa kufanyika Jumamosi lakini yakaahirishwa kutokana na kile Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) ilisema kuwa “hitilafu za kimipango.”

Badala yake, maafisa wa idara hiyo walisema upasuaji huo utafanyika kesho Jumanne.

Bi Kangogo, 34, anadaiwa kufariki baada ya kujipiga risasi kichwani nyumbani kwao katika eneo la Nyawa, Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

“Tutapanga mazishi hayo kikamilifu baada ya DCI kutoa ripoti ya upasuaji,” alieleza Bw Robert Kipkorir, msemaji wa familia hiyo.

Afisa Mkuu wa DCI katika kaunti hiyo, Bw Alfred Majimbo, alisema shughuli ya upasuaji wa mwili wa marehemu inasimamiwa na makao makuu ya idara hiyo.

“Tunangoja mpasuaji wa serikali kufika ili kutekeleza kazi hiyo,” akaeleza Bw Majimbo.

Kulingana na familia, upasuaji huo utafanyika Jumanne kufuatia makubaliano na maafisa wa DCI.

“Hatuna jingine ila kungoja ripoti ya upasuaji wa mwili, ndiposa tuweke mipango yoyote ya mazishi,” aliongeza babake marahemu, Bw Barnabas Kibor.

Familia ilieleza kusikitishwa na hatua ya maafisa wa DCI eneo hilo kuwazuia kuchukua mwili wa mwana wao kwa mazishi ya Jumamosi kama ilivyokuwa imepangwa.

“Tulikuwa tumekubaliana na DCI kuhusu taratibu za upasuaji na mipango ya mazishi. Sielewi ni kwanini ninazuiwa kuchukua mwili wa mwanangu ili kwenda kuuzika,” alihoji Bw Kibor huku akibubujikwa na machozi.

Kwa mara ya kwanza tangu kifo cha konstebo Kangogo familia iliandikisha taarifa kuhusu kifo chake katika afisi za DCI mjini Iten.

“Nilikuwa katika afisi za DCI leo asubuhi pamoja na mwanangu Mark Kangogo, kuandikisha taarifa kama inavyohitajika. Kilichopaswa kufuata ni idara kutoa ripoti ya upasuaji na kisha kuachiliwa kwa mwili wa marehemu. Hata hivyo, nilishangazwa sana na mwelekeo ambao matukio yamechukua,” alieleza Mzee Kibor aliyewahi kuhudumu kama inspekta wa polisi.

Familia hiyo ilikuwa imeshanunua jeneza tayari kuuchukua mwili.

Hata hivyo, hilo halikutimia kwani mwali haukuwa umefanyiwa upasuaji.

Kakake marehemu, Mark, alisema kile familia hiyo inataka kukabidhiwa mwili wa mpendwa wao akidai wanashuku njama fiche katika ucheleweshaji wa upasuaji huo.

“Inasikitisha kuwa tunazuiwa kuchukua mwili wa jamaa yetu ilhali mipango yote ya mazishi imekamilika. DCI ilifaa kutuambia mapema kuhusu mabadiliko yoyote,” akasema.

Kangogo ulipatikana ndani ya bafu lao, umbali wa mita 40 kutoka nyumba ya wazazi wake, akiwa amefariki.

You can share this post!

Polisi wadaiwa kurusha kilipuzi katika baa

MAKALA MAALUM: Mahangaiko tele ya kupata tiba yalazimu...