• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
TAHARIRI: Bunge liharakishe sheria ya umasikini

TAHARIRI: Bunge liharakishe sheria ya umasikini

KITENGO CHA UHARIRI

HALI ngumu ya uchumi inayosababishwa na janga la corona, imesababisha Wakenya wengi kuendelea kudidimia katika lindi la umasikini.

Kuangamiza umasikini ni lengo la kwanza kati ya Malengo 17 ya Maendeleo (SDGs). Baada ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia ambayo pia yalihusisha kuangamiza umasikini, Umoja wa Mataifa ulitaka kusiwe na umasikini kabisa ifikapo mwaka 2030.

Jijini Nairibi familia zinazoishi barabarani zimeililia serikali kuwa zinakumbwa na njaa. Watu watatu wa familia hizo walifariki dunia wiki kwa kukosa chakula na dawa baada ya kuugua.

Tatizo la njaa si la familia za kurandaranda mitaani pekee. Mamilioni ya Wakenya wanaishi katika mazingira magumu, hasa baada ya kupanda kwa bei za bidhaa muhimu. Tangu Julai 1, bejeti ilipoanza kutekelezwa, bei za bidhaa zinazotumiwa na mwananchi zilianza kupanda.

Takwimu mbalimbali ikiwemo ile ya Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS), zinaonyesha kiwango cha umasikini nchini kinaendelea kupanda.

Kinyume na awali ambapo umasikini ulikuwa mashambani, sasa hivi idad kubwa ya watu walio mijini ni masikini kupindukia.

Kwa hivyo, ilitarajiwa kuwa kungekuwa na mikakati ya kurekebisha hali hii.

Mojawapo ya mikakati hiyo ni kupitia sheria maalumu ambayo ingebuni bodi ya kudhibiti umasikini. Harakati hizo zilianzishwa na kuundwa kwa Mswada wa Kubuniwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti Umasikini, 2020.

Sheria hiyo ingehakikisha kwamba kuna mamlaka inayoangazia masuala ya umasikini na kutoa mapendekezo kwa serikali na wadau wengine kuhusu jinsi ya kukabiliana nao.

Lakini kuna hofu kuwa huenda hilo lisitimie. Mswada huo ni miongoni mwa mingine 59 ambayo imekwama bungeni katika hatua mbalimbali.

Sheria hiyo huenda isipitishwe hivi karibuni, ikizingatiwa kuwa kumesalia karibu mwaka mmoja pekee kabla ya Bunge kuvunjwa.

Isitoshe, wabunge wameanza kukodolea macho kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao, zinazotarajiwa kung’oa nanga mwezi Mei.

Kwa sababu hiyo, kuna haja kwa Spika Justin Muturi na uongozi wa Bunge kwa jumla kuwahamasisha wabunge kuharakisha mswada huo. Kupitishwa mswada wa kubuni mamlaka ya Kudhibiti Umasikini itakuwa zawadi kubwa zaidi kwa mwananchi.

You can share this post!

WASONGA: Masomo yasivurugwe tena mwaka huu mfupi

Benki ya Equity yafadhili wanafunzi 167 Kiambu