• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Pendekezo vyeti vya kuzaliwa vitumike kusajili wapigakura

Pendekezo vyeti vya kuzaliwa vitumike kusajili wapigakura

Na ALEX KALAMA

MAPENDEKEZO ya kutaka wananchi waruhusiwe kutumia vyeti vya kuzaliwa kujisajili kupiga kura yanaendelea kutolewa huku kukiwa na malalamishi kuhusu ugumu wa vijana kupata vitambulisho vya kitaifa.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imethibitisha kupokea mapendekezo aina hiyo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wanaotaka wananchi walio na umri wa zaidi ya miaka 18 waruhusiwe kutumia vyeti vya kuzaliwa kujiandikisha kupiga kura.

Kisheria, mtu anayetaka kujisajili kuwa mpigakura huhitajika kuwa na kitambulisho cha kitaifa au paspoti halali.

Msimamizi mkuu wa IEBC katika Kaunti ya Kilifi, Bw Abdul Wahid Hussein, alisema wito huo wa wanasiasa tayari umekuwa ukiungwa mkono na baadhi ya wananchi.

Hata hivyo alisisitiza kuwa kwa sasa mfumo huo hauwezi kutumiwa kwani sheria za uchaguzi haziruhusu.

“Tumepokea mapendekezo ya baadhi ya wananchi kwamba wale vijana walio na umri wa zaidi ya miaka 18 wasajiliwe kuwa wapigakura kwa kutumia vyeti vya kuzaliwa. Tunataka kuwaambia kwamba vyeti hivyo vinakosa baadhi ya matakwa yanayohitajika ili kumsajili mtu kuwa mpigakura,” alisema Bw Hussein.

Mapendekezo hayo yalikuwa yametolewa na baadhi ya wanasiasa wakiongozwa na diwani wa wadi ya Gongoni, Bw Albert Kiraga na Kiongozi wa Chama cha Kadu Asili, Bw Gerald Thoya.

Wanaounga mkono pendekezo hilo walidai kuwa inawezekana kutumia vyeti hivyo kwa vile ndivyo hutumiwa na serikali kuwasajili watahiniwa wa mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE bila dosari.

Bw Thoya vile vile alisema kumekuwa na ulegevu katika ofisi husika ya usajili wa vitambulisho, hali inayowafanya wakazi wengi kususia kuenda kuchukua vitambulisho vyao.

“Endapo IEBC itakubali ombi hilo basi wananchi wengi watakumbatia mpango huo wa kujisajili kupiga kura,” akasema.

Wiki iliyopita wakati wa mahojiano ya wawaniaji nafasi ya kamishna wa IEBC, wakili Florence Jaoko aliyehojiwa kwa wadhifa huo pia alitoa pendekezo sawa na hilo.

Bw Hussein alieleza matumaini kuwa wananchi wengi watajitokeza kujiandikisha kupiga kura katika Kaunti ya Kilifi kabla uchaguzi wa mwaka ujao.

Wakati huo huo, Chama cha Kadu Asili kinawataka viongozi wa kisiasa kupunguza cheche za maneno ambazo huenda zikaleta migawanyiko miongoni mwa wananchi.

Akizungumza afisini mwake mjini Malindi, Bw Thoya alionya kuhusu joto la kisiasa na kuhimiza viongozi kuazimia zaidi kuunganisha taifa.

Bw Thoya alishauri jamii kujiepusha na wanasiasa wachochezi wakati huu taifa hili linapojianda kwa uchaguzi wa mwaka wa 2022 na kudumisha umoja.

“Ningependa kuwasihi wananchi wote kuwaepuka viongozi wachochezi ambao wanakataa juhudi za kudumisha umoja. Pia navisihi vitengo husika kulishughulikia swala hilo,” alisema Bw Thoya.

You can share this post!

Mumias: Wabunge wataka mrasimu atoe ripoti ya mapato

Uchaguzi: EACC yataka watumishi wajiuzulu kwanza