• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa Kiambu washauriwa kukumbatia mfumo wa silage

Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa Kiambu washauriwa kukumbatia mfumo wa silage

Na SAMMY WAWERU

WAFUGAJI wa ng’ombe wa maziwa Kaunti ya Kiambu wamehimizwa kukumbatia mfumo wa kuhifadhi malisho na lishe kwa minajili ya matumizi ya baadaye.

Gavana James Nyoro amesema mfumo wa silage utawawezesha kuepuka mahangaiko ya upungufu wa lishe wakati wa kiangazi.

Silage, ni mfumo wa kuvuna malisho ya mifugo kama vile nyasi za mabingobingo, majani na matawi ya nafaka na nyasi zinginezo, zikiwa mbichi kisha kuzifunika kuzuia hewa kuingia na kuzihifadhi.

Aidha, hazikaushwi ili kudumisha kiwango cha madini na virutubisho.

“Kiambu ni mzalishaji wa nafaka. Wakulima ambao ni wafugaji wanapovuna mahindi, wahifadhi majani na matawi yake kupitia mfumo wa silage,” Bw Nyoro akashauri.

Akiusifia, gavana alisema wataalamu wa masuala ya mifugo wamethibitisha malisho yaliyohifadhiwa kwa njia hiyo yanaongeza kiwango cha maziwa.

“Isitoshe, mfugaji atakuwa amepunguza mahangaiko ya lishe wakati wa kiangazi na pia gharama ya kununua chakula cha madukani,” akasema.

Gavana Nyoro alisema wakulima na wafugaji wakitilia maanani mfumo huo, Kiambu itaendelea kuorodheshwa kuwa mzalishaji mkuu wa maziwa nchini.

Chakula cha madukani, alishauri wafugaji kukinunua kutoka kwa watengenezaji walioidhinishwa na asasi husika ili kukwepa kero ya kile duni na ambacho hakijaafikia ubora wa bidhaa.

  • Tags

You can share this post!

Uchaguzi: EACC yataka watumishi wajiuzulu kwanza

Kalonzo avua kivuli cha Raila