• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:21 PM
Maskini kuongezeka hadi milioni 490 barani Afrika

Maskini kuongezeka hadi milioni 490 barani Afrika

Na MASHIRIKA

KAMPALA, Uganda

IDADI ya maskini inatarajiwa kuongezeka barani Afrika katika miaka 10 ijayo, kulingana na ripoti ya shirika moja la Umoja wa Mataifa (UN).

Ripoti hiyo iliyotolewa na sekretariati inayosimamia Malengo ya Maendeleo (SDG) ya Umoja wa Mataifa, inasema kuwa idadi ya watu wanaohangaika kupata mahitaji ya kila siku itaongezeka kutoka milioni 400 hadi 490 kufikia 2030.

Hiyo inamaanisha kuwa, asilimia 80 ya maskini kote duniani watapatikana barani Afrika, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Aidha, asilimia 75 ya maskini wanaishi vijijini ambapo wengi wanatatizika mno kupata chakula, malazi na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

“Iwapo serikali za Afrika hazitajikakamua kuboresha uchumi, hali itakuwa mbaya zaidi katika miaka 10 ijayo,” inaeleza ripoti hiyo.

Kati ya mataifa 36 ambayo yameorodheshwa kuwa maskini zaidi ulimwenguni, 33 yako barani Afrika.

Ripoti inasema kuwa uchumi wa mataifa mengi ya Afrika umedorora, jambo ambalo limesababisha ongezeko la watu wasio na kazi.

“Hata wanaofanya kazi wanapata ujira duni unaowafanya kuendelea kuzama katika umaskini,” inaongeza.

Janga la corona limetajwa kama lililoongezea nchi za Afrika masaibu zaidi ya kiuchumi.

Kulingana na utafiti wa Benki ya Dunia uliotolewa mwaka jana, asilimia 70 ya maskini Afrika wanapatikana Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ethiopia, Tanzania, Kenya, Madagascar, Msumbiji, Uganda na Malawi.

Utafiti huo unasema kuwa matajiri wanapata huduma bora za matibabu na elimu huku maskini wakipata duni.

“Ili kuleta usawa, maskini wanafaa kuwezeshwa kupata huduma bora za matibabu, makazi na elimu,” ripoti ya utafiti huo inasema.

Inaeleza kwamba itakuwa vigumu kwa Afrika kutimiza malengo ya SDG ya kumaliza umaskini kufikia 2030.

Kumaliza umaskini ni moja ya malengo 17 ya SDG ambayo UN inataka kuyatimiza kufikia 2030.

Hii ikiwemo kumaliza njaa, kuwepo usawa wa kijinsia na kuboresha huduma za afya.

Kwa mujibu wa ripoti ya UN, ni mataifa mawili pekee – Mauritania na Gabon, ambayo yanapambana vikali kupunguza umaskini.

Kinaya ni kwamba watu milioni 16 (asilimia 26) nchini Afrika Kusini wanaishi katika umaskini, ilhali taifa hilo ndilo la pili kwa utajiri mkubwa barani Afrika.

Watu milioni 90 (asilimia 40) wamezama katika umaskini nchini Nigeria, licha ya nchi hiyo kuongoza kwa utajiri kote Afrika.

Mataifa maskini zaidi barani ni Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Madagascar na DRC.

You can share this post!

Tundo sasa aongoza jedwali la Mbio za Magari Afrika baada...

MAKALA MAALUM: Matunda ya elimu yamsukuma kuwa mtetezi sugu...