• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 3:04 PM
MAKALA MAALUM: Matunda ya elimu yamsukuma kuwa mtetezi sugu wa mabinti

MAKALA MAALUM: Matunda ya elimu yamsukuma kuwa mtetezi sugu wa mabinti

Na KALUME KAZUNGU

KWA miaka mingi, jamii ya Wabajuni imekuwa mojawapo ya zile zinazosifika kwa tamaduni zao zinazofanya Lamu iwe kivutio cha watalii, wanaotaka kushuhudia desturi za kiasili za ufuoni.

Hata hivyo, sawa na jamii nyingine zilizoshikilia desturi zao za jadi, jamii hiyo imekuwa ikikumbwa na malalamishi kutoka kwa baadhi ya wasomi na wanajamii kuwa desturi nyingine zimepitwa na wakati na zinastahili kuzikwa katika kaburi la sahau.

Huenda ikawa ni miito hii ambayo imefanya sasa kuwe na idadi kubwa kiasi cha haja cha wasichana na wanawake ambao wanaendeleza masomo yao kwa kiwango kinachowawezesha kupata ajira ambazo zilidhaniwa kuwa za wanaume pekee katika miaka ya iliyopita.

Katika lokesheni ya Matondoni iliyo tarafa ya Amu, tulikutana na Bi Ruhia Shee Mohamed ambaye ndiye chifu wa kwanza mwanamke wa asili ya Kibajuni.

Bi Ruhia Shee Mohamed, 34, ambaye ni mama wa mtoto mmoja aliingia orodha ya kuwa chifu mwanamke wa kwanza kutoka jamii ya Wabajuni wa Lamu kushikilia wadhfa huo.

Alipata kazi hiyo mnamo Juni 30, 2017 baada ya kuhitimu masomo yake ya Masuala ya Usimamizi na Uajiri wa Wafanyakazi katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM).

Bi Ruhia alizaliwa katika Kijiji cha Matondoni, akajiunga na Shule ya Msingi ya Matondoni kabla ya kuhamishwa hadi kwenye shule ya wasichana ya Msingi ya Mjini Lamu alikomalizia masomo yake ya msingi.

Baadaye alijiunga na Shule ya Upili ya Wasichana ya Lamu alikohitimu mnamo 2006.

Kuajiriwa kwake kuwa karani wa chifu wa Matondoni mnamo Januari, 2008 kulimpa motisha kubwa kwamba ana uwezo wa kutekeleza majukumu makubwa zaidi ya kiusimamizi

Bi Ruhia anasema baada ya ndoto yake ya kuwa chifu kutimia, mafanikio yake yalimchochea kujitolea kutetea haki za jinsia ya kike.

Aliamua kujitolea kupigania haki za jinsia ya kike ambazo zilikuwa zimetelekezwa kwa miaka mingi, hasa mwanamke wa Kibajuni ambaye tangu jadi amekuwa akidhalilishwa na kuonekana tu kuwa chombo cha kutekeleza majukumu ya nyumbani kamavile kulea watoto na kupikia waume zao.

“Jamii yetu ya Kibajuni haijazingatia sana masilahi ya jinsia ya kike. Hii ndiyo sababu wanawake wengi wameishia kuolewa mapema, kuzaa na kukaa nyumbani. Mimi nimepata wadhifa huu wa chifu ambao ninautumia kudhihirishia jamii yangu kwamba mwanamke wa Kibajuni pia aweza kutekeleza majukumu ya kiofisi na kusaidia mumewe kutafuta na kuleta chakula kwa meza,” akasema Bi Ruhia.

Chifu huyo pia amejitolea kuhimiza jamii kuzingatia masomo kwa wasichana.

Anasema kabla ya kupata wadhfa huo, lokesheni ya Matondoni ilikuwa ikiongoza kwa visa vya ndoa za mapema na mimba zisizohitajika.

Ijapokuwa serikali kuu iliagiza machifu kitaifa wawe katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya ndoa na mimba za wasichana walio na umri wa chini ya miaka 18, kuna maeneo mengi ambayo yamelemewa na visa hivyo bado vimekithiri.

Lakini Bi Ruhia anaamini kuwa, kupitia mchango na bidii zake kupigania haki za wanawake, wasichana wengi kutoka eneo lake wamejiunga na shule na vyuo vya elimu ya juu kusoma.

“Tuko na idadi kubwa ya wasichana ambao wamejiunga na shule za msingi, upili, taasisi na vyuo kusomea kozi mbalimbali. Yote haya yanatokana na msukumo wangu katika jamii kwamba izingatie sana elimu ya mtotowa kike,” akasema Bi Ruhia.

Kando na kujali masilahi ya wasichana wadogo, chifu huyo pia amejitwika jukumu la kutatua mizozo ya nyumbani ili kukabiliana na visa vilivyokuwa vimekithiri vya talaka.

Anasema kila mara amekuwa akikaa na wanawake na pia wanaume na kushauriana nao kuhusiana na jinsi wanavyopaswa kutunza ndoa zao.

“Katika miaka ya awali, lokesheni ya Matondoni ilikuwa na visa vingi vya talaka. Talaka zilikuwa zikitolewa ovyo ovyo. Leo hii nikisimama hapa, visa vya talaka vimepungua kwa kiwango kikubwa,” akasema Bi Ruhia.

Licha ya kukumbana na changamoto za machifu wenzake wanaume ambao awali walikuwa wakimdharau na kumchukulia kwamba hawezi kazi hiyo, anatabasamu kuwa wengi kwa sasa wamemkubali na kumpigia saluti kwa utendakazi wake sufufu anaodhihirisha.

Baadhi ya machifu, hasa wanaume waliozungumza na Taifa Leo walimsifu Bi Ruhia kuwa mwanamke ngangari na mwenye bidi kazini.

Mwenyekiti wa machifu wa Lamu, ambaye pia ni chifu wa Mkomani, Bw Masjid Basheikh alimtaja Bi Ruhia kuwa mtu muadilifu, mwenye kujitolea kazini na asiyeogopa.

“Mimi hufurahia sana nikifanya kazi na Bi Ruhia. Yeye ni mchesi, mtu wa heshima na mwenye kujitolea kwa bidi kazini,” akasema Bw Basheikh.

Kulingana na Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Kaunti ya Lamu, Ruweida Obbo, wanawake wengi, hasa wa asili ya Kibajuni wamekuwa wakikimbilia nyadfha za chini na rahisi kama vile ile anayoshikilia, udiwani au hata kusubiri kuteuliwa kama viongozi maalum kwenye nyadhifa za kisiasa kwa kuhofia kusutwa na jamii.

Bi Obbo ambaye sasa amepanga kuwania ubunge Lamu Mashariki, anawahimiza wanawake wenzake kuacha woga na badala yake kujikaza, wajitose ulingoni ili kupigania nyadhfa kubwa za uongozi.

Aidha, mwanamke wa Kibajuni ambaye kwa sasa ametangaza azma ya kuwania nyadfha ya juu kwa mara ya kwanza katika historia ambayo ni ugavana wa Lamu ifikapo uchaguzi mkuu wa 2022 ni Bi Umra Omar, 37.

Bi Obbo anasema ni kupitia idadi kubwa ya wanawake kuwa uongozini ambapo usawa, haki, uongozi bora na maendeleo yataafikiwa Lamu na nchini kwa ujumla.

“Nitafurahi zaidi endapo nitaona wanawake wenzangu wakipigania nyadfha kubwa, hata ugavana hapa kwetu. Tuache kukimbilia nyadhfa ndogo ndogo eti kwa sababu sisi ni wanawake. Tupiganie usawa na uwajibikaji,” akasema Bi Obbo.

Baadhi ya wanawake wa asili ya Kibajuni waliohojiwa na Taifa Leo walikiri kuwa mbali na kuogopa kusutwa na wanaume wanapojitokeza kupigania vyeo hasa vya kisiasa, wanawake wenyewe kwa wenyewe pia wamekuwa maadui na kizingiti katika kupigania nyadhfa kubwa kubwa Lamu.

“Jamii inakuona wewe mwanamke kama mtu aliyepotoka kimaadili. Unatukanwa kichinichini. Wanawake wenzako pia hukunyima kura maksudi kwa sababu hawaamini kwamba jinsia ya kike pia inaweza kuongoza. Wanaamini uongozi wa wanaume,” akasema Bi Amina Bakari.

You can share this post!

Maskini kuongezeka hadi milioni 490 barani Afrika

TAHARIRI: Suluhu yahitajika shule za sekondari