• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
ODONGO: Mudavadi na Kalonzo hawawezi kitu bila Raila

ODONGO: Mudavadi na Kalonzo hawawezi kitu bila Raila

Na CECIL ODONGO

MSUKUMO wa baadhi ya viongozi wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kujiondoa katika NASA unachochewa na dhana kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kumkata mguu kisiasa kinara wa ODM, Raila Odinga na kulipiza kisasi kwa kukataa kuwaunga mkono 2022.

Vyama tanzu ndani ya Nasa vinatarajiwa kurasimisha mchakato wa kujiondoa kwenye Nasa ambayo ilivunia Bw Odinga zaidi ya kura milioni sita katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Wiper inayoongozwa na Kalonzo Musyoka, Ford Kenya yake Moses Wetang’ula na ANC ya Musalia Mudavadi, vyote vinatarajiwa kupitisha azimio la kujiondoa katika Nasa kwenye mkutano wa Baraza Kuu la vyama hivyo wiki hii.

Kati ya sababu ambazo zinadaiwa kuchangia kuporomoka kwa Nasa ni hatua ya ODM kukataa kutoa mgao wa fedha za vyama vya kisiasa kwa washirika wake na hatua ya Bw Odinga kukataa kumuunga mkono mwaniaji mwengine ndani ya NASA kwa mujibu wa mkataba ulioafikiwa kabla ya kura ya 2017.

Hata hivyo, huenda tamaa ya uongozi wa wanasiasa hawa watatu ndiyo imechangia wao kujiondoa katika Nasa ilhali hawana uungwaji mkono wowote wa maana unaoweza kuwawezesha kushinda kiti cha urais.

Swali, hata hivyo, ni je baada ya kujiondoa Nasa na kubuni OKA, wataimarisha nafasi yao ya kushinda kiti cha urais?

Ingawa wametangaza kuwa watashirikiana na mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi ndani ya OKA, huenda ikawa vigumu kwa Bw Musyoka na Bw Mudavadi kuelewana kuhusu ni nani kati yao anayefaa kupeperusha bendera ya muungano huo.

Bw Wetang’ula ni mwanasiasa ambaye hana ushawishi wowote wa maana isipokuwa ndani ya kaunti za Bungoma na Trans Nzoia pekee. Kwa hivyo, hayuko katika hesabu za kuwania urais katika muungano huo.

Hali ni hiyo kwa Bw Moi ambaye licha ya ukwasi mkubwa, pia hawezi kutoa ushindani wa maana kwa Naibu Rais, Dkt William Ruto hasa katika eneo la Bonde la Ufa.

Mabw Musyoka na Mudavadi nao wameona kuwa farasi wawili 2022 ni Bw Odinga na Dkt Ruto, kwa hivyo, wanajaribu kujidhihirisha kuwa hata wao ni majabari.

Hata hivyo, iwapo watakubaliana mmoja awe mwaniaji wa urais na mwengine mwaniaji mwenza, itakuwa vigumu kwao kuungwa mkono nje ya Ukambani na Magharibi.

Kwa kuwa nia yao kuu ya kujiondoa Nasa ni kusaka urais, ni vyema wote waelekee kwenye debe na wajiabishe kwa kupata kura chache ambazo zitawaweka kwenye baridi kisiasa kwa miaka mingine mitano.

Ndiyo ni kweli Bw Odinga ana nafasi nzuri ya kumbwaga Dkt Ruto 2022 iwapo atasalia na viongozi waliomuunga mkono 2013 na 2017, ila kuondoka kwao kunampa nafasi ya kuwasaka washirika wapya ambao wanaweza kuongeza kura zake bila vigogo hao.

Badala ya kutoroka Nasa na kuendelea kusaka kura kivyao, viongozi wa OKA wanafaa watafakari na wajiunge na mrengo wa Dkt Ruto au Bw Odinga kwa kuwa hawawezi kumudu ushindani unaotolewa na wawili hao wenye ufuasi mkubwa nchini.

Mwishowe wakielekea debeni na mgawanyiko kama huu uendelee, basi Dkt Ruto ana nafasi nzuri ya kupenya hadi ikulu kuliko hata Bw Odinga.

Itakuwa kama 1992 ambapo upinzani uligawanyika kutokana na tamaa ya uongozi naye Rais Daniel arap Moi akatetea kiti chake kwa urahisi katika kura ya kwanza ya mfumo wa vyama vingi nchini.

La muhimu ni kwamba msukomo wa kulipiza kisasi dhidi ya Bw Odinga haufai utumike na Mabw Mudavadi, Musyoka na Wetang’ula kujizika zaidi katika kaburi la kisiasa.

Wakubali tu kuwa bado wana safari ndefu kupata uungwaji mkono mkubwa kama wa Bw Odinga au Dkt Ruto badala ya kukimbia kuwania urais wakifahamu vizuri watakuwa tu washiriki wala hawana nafasi ya kutua ikuluni.

You can share this post!

TAHARIRI: Suluhu yahitajika shule za sekondari

WANGARI: Mfumo jumuishi kwa watoto wote utaokoa elimu Kenya