• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
WANGARI: Mfumo jumuishi kwa watoto wote utaokoa elimu Kenya

WANGARI: Mfumo jumuishi kwa watoto wote utaokoa elimu Kenya

Na MARY WANGARI

SHULE zinapofunguliwa juma hili kwa Muhula wa Kwanza mwaka huu, ni wazi kuwa mageuzi muhimu yanahitajika ili kuepuka kuongezeka kwa ukosefu wa usawa katika sekta ya elimu nchini.

Sekta ya elimu ni miongoni mwa nyanja ziliozoathirika zaidi nchini kutokana na janga la Covid-19 lililozuka karibu miaka miwili iliyopita.

Hata baada ya serikali kujitahidi kwa hali na mali kuwezesha taifa kurejelea hali ya kawaida, nyanja ya elimu bila shaka ina mwendo mrefu kabla ya kupata nafuu kikamilifu kutokana na athari za baada ya ugonjwa wa Covid-19.

Kuanzia ratiba za mihula zinazoonekana kuwakanganya wazazi na wanafunzi, karo ya shule na malipo ya ziada yanayozidi kupanda, matatizo ya kiakili na kisaikolojia kwa wazazi na watoto kutokana na shinikizo mbalimbali, ni baadhi tu ya masaibu yanayowakosesha Wakenya wengi usingizi hasa katika msimu huu wa shule kufunguliwa baada ya likizo ya wiki moja.

Licha ya Wizara ya Elimu kujitahidi kuhakikisha watoto wote wamerejea shuleni, uhalisia ni kuwa, kwa wanafunzi wengi hasa kutoka mashinani, imekuwa vigumu mno kurejelea shughuli za masomo na maisha ya kawaida.

Tafiti kadhaa nchini na kimataifa tayari zimeonyesha athari ya kufunga shule dhidi ya zinapokuwa zimefunguliwa, miongoni mwa wanafunzi.

Kulingana na wataalam kuhusu masuala ya elimu, wanafunzi hasa walio katika madarasa ya chini na maeneo ya mashinani hurudi nyuma kimasomo shule zinapofungwa.

Ikizingatiwa kwamba ndio mwanzo tu wanafunzi wamerejea shuleni kufuatia likizo ya zaidi ya miezi kumi, ni bayana kwamba wadau husika wanahitajika kujikakamua zaidi.

Isitoshe, hatua zilizopigwa kuwezesha usawa katika sekta ya elimu zinakabiliwa na tishio huku takwimu zikidhihirisha uhalisia wa kuhofisha.

Ripoti zinaashiria kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wa kike wameathirika kielimu kushinda wavulana kutokana na masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

Kwa upande mwingine, wanafunzi wanaoishi vijijini wameathirika pakubwa ikilinganishwa na wenzao wanaoishi mijini walio na umeme, intaneti na uwezo wa kuendeleza masomo yao kidijitali.

Umuhimu wa mageuzi katika mfumo wa elimu hususan kujumuishwa kikamilifu kwa elimu kidijitali kwa kuwezesha kila mwanafunzi kupata huduma za intaneti, ni mkubwa usio na kifani.

Kenya, kama taifa mwanachama wa Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu Kufanikisha Elimu Kidijitali, ni sharti ijitahidi kufanikisha Azimio la 2030 kuhusu kuunganisha intaneti katika shule zote za umma nchini.

Mikakati ya muda mrefu inahitajika, vilevile, ili kufanikisha mifumo jumuishi ya kielimu kuambatana na viwango vya kisasa duniani.

Kongamano la Kimataifa kuhusu Elimu Duniani litakaloandaliwa na Kenya pamoja na Uingereza ni fursa muhimu kwa viongozi wa kimataifa, ikiwemo Kenya, kubuni mikakati madhubuti itakayohakikisha kila mtoto anapata haki yake ya elimu bora.

[email protected]

You can share this post!

ODONGO: Mudavadi na Kalonzo hawawezi kitu bila Raila

SHINA LA UHAI: Huduma mbovu katika hospitali za Kaunti...