• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:55 PM
Onkar Rai aibuka mwanamichezo bora Kenya mwezi Juni

Onkar Rai aibuka mwanamichezo bora Kenya mwezi Juni

Na AGNES MAKHANDIA

DEREVA mkazi wa Kaunti ya Nakuru, Onkar Rai ndiye mshindi wa mwezi Juni wa tuzo ya mwanamichezo bora wa Chama cha Waandishi wa Michezo (SJAK) inayodhaminiwa na kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya LG.

Onkar, ambaye alifichua jana kuwa hatashiriki duru ijayo ya Mbio za Magari za Kitaifa za Kenya (KNRC) mnamo Agosti 7-8, alituzwa baada ya kung’ara katika duru ya sita ya Mbio za Magari Duniani (WRC) Safari Rally mnamo Juni 24-27.

Dereva huyo mwenye umri wa miaka 33, alimaliza Safari Rally nyuma ya bingwa wa dunia Sebastien Ogier (Ufaransa), Takamoto Katsuta (Japan), Ott Tanak (Estonia), Gus Greensmith (Uingereza), Adrien Fourmaux (Ufaransa) na Kalle Rovanpera (Finland).

Hapo Julai 26, Onkar, ambaye alielekezwa na Muingereza Drew Sturrock wakiendesha gari la Volkswagen Polo R5, alizawadiwa runinga ya inchi 55 ya LG Nanocell ambayo bei yake sokoni ni Sh120,000.

Onkar aliamua kupeana runinga hiyo kwa hospitali ya Nakuru ili kusaidia katika kuhamasisha watu kuhusu jeraha la uti wa mgongo.

Alibwaga mwanaolimpiki Brackcides Agala (voliboli ya ufukweni) na watimkaji Ferdinand Omanyala (mita 100), Faith Kipyegon (mita 1,500), Geoffrey Kamworor (mita 10,000) na chipukizi wa mpira wa vikapu Medina Okot.

“Ni heshima kubwa kutunukiwa zawadi na inathibitisha kuwa nimekuwa nikifanya nzuri na pia kujitolea kwa miaka miwili iliyopita. Singepata matokeo hayo mazuri bila ya kuwa na watu wanaonisaidia karibu name akiwemo ndugu yangu Tejveer (Rai) na babangu Jaswant,” alisema Onkar.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

Wanasoka 10 wa Pwani kupigania nafasi Starlets U-20

Lynn anaamini ipo siku watakubali kazi yake katika uigizaji