• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 5:39 PM
Wafugaji na wafanyabiashara wahimizwa kutathmini namna ya kusafirisha mifugo

Wafugaji na wafanyabiashara wahimizwa kutathmini namna ya kusafirisha mifugo

Na SAMMY WAWERU

WAFUGAJI na wafanyabiashara wametakiwa kutathmini mbinu wanazotumia kusafirisha mifugo yao.

Dkt Victor Yamo kutoka shirika la kimataifa linaloangazia masuala ya mifugo na wanyamapori – World Animal Protection – amesema mbinu nyingi zinazotumika nchini kusafirisha mifugo zinakiuka haki za wanyama.

Vilevile, mdau huyu amesema zinachangia kudhoofika na kudorora kwa ubora wa mazao ya mifugo.

“Kwa hakika, unapotazama wanavyosafirishwa mifugo wakipelekwa vichinjioni, haki zao zinakiukwa,” Dkt Yamo akasema akielezea hofu kuhusu mbinu zinazotumika.

Licha ya mifugo kupelekwa kwenye buchari kwa minajili ya kuchinjwa, alisema wana haki kisheria kusafirishwa kwa njia ya heshima.

“Maslahi ya mifugo ni muhimu na yanapaswa kuheshimiwa. Nyakati zingine utaona mfugo amefungwa kikatili, akipelekwa kichinjioni.

Ni muhimu tufahamu kuwa ubora wa mazao yake pia unategemea anavyosafirishwa. Nyama za hadhi ya chini zinatokana na jinsi anabebwa,” akasema.

Dkt Yamo alisema hayo Jumanne, kwenye mafunzo ya wanahabari kwa njia ya mtandao wa Zoom yaliyoandaliwa na World Animal Protection kwa ushirikiano na Baraza la Vyombo vya Habari Nchini Kenya (MCK).

Amehimiza wanahabari kujituma na kuangazia jinsi mifugo husafirishwa, Dkt Yamo pia alieleza haja ya wahudumu wa buchari kujiri na mikakati bora ya uchinjaji.

“Kuna vigezo vya kimataifa vilivyowekwa kuhusu maslahi ya mifugo. Tuvitambue na kuviheshimu,” akasisitiza.

You can share this post!

Rashford ataka fedha zilizochangishwa na mashabiki...

Wito wagonjwa wa kawaida wazuru hospitali nyinginezo idadi...