• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Helena Alcinda Panguana ampangua Mkenya Elizabeth Akinyi kwa njia ya TKO

Helena Alcinda Panguana ampangua Mkenya Elizabeth Akinyi kwa njia ya TKO

Na GEOFFREY ANENE

MABONDIA wote waliofuzu kuwakilisha Kenya kwenye Olimpiki 2020 wamebanduliwa baada ya Elizabeth Akinyi kuwa wa mwisho kupigwa jijini Tokyo, Japan mnamo Julai 27.

Akinyi amepanguliwa na Alcinda Helena Panguana kutoka Msumbiji katika raundi ya kwanza kwa njia ya TKO katika pigano la lake la kwanza la raundi ya 16-bora la uzani wa kilo 64-69 (welter) katika ukumbi wa Kokugikan.

Mwanamasumbwi huyo mwenye umri wa miaka 27 alikutana na Panguana katika mashindano ya Afrika ya ukanda wa tatu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwezi Machi na kulimwa.

Akinyi alishuka jukwaani saa chache baada ya Elly Ajowi Ochola kutandiwa makonde mazito na Julio la Cruz kutoka Cuba akipoteza kwa alama 5-0 katika pambano la uzani wa kilo 81 hadi kilo 91 (Heavy) katika raundi ya 16-bora.

Mkenya wa kwanza kuaga mashindano alikuwa Nick “Commander” Okoth aliyelemewa na Tsendbaatar kutoka Mongolia 3-2 katika mchuano wa raundi ya 32-bora wa uzani wa unyoya (kilo 52-57) mnamo Julai 24.

Christine Ongare alifuata mkondo huo aliponyukwa 5-0 na Irish Magno kutoka Ufilipino katika mechi ya raundi ya 32-bora ya uzani wa kilo 48-51 (Fly).

Mara ya mwisho Kenya ilishinda medali ya ndondi kwenye Olimpiki ilikuwa mwaka 1988 jijini Seoul nchini Korea Kusini kupitia kwa Robert Wangila (dhahabu ya uzani wa welter) na Chris Sande (fedha ya uzani wa kati).

You can share this post!

Bermuda yawa nchi ya kwanza ndogo zaidi kuwahi kuzoa medali...

Tufundishwe jinsi ya kuvua samaki na si kuletewa samaki,...