• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 9:55 AM
Wanasoka 10 wa Pwani kupigania nafasi Starlets U-20

Wanasoka 10 wa Pwani kupigania nafasi Starlets U-20

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

WANASOKA 10 wa eneo la Pwani wamefuzu kuchaguliwa kwenda kwa majaribio ya timu ya kitaifa ya soka ya wasichana ya Harambee Starlets itakayoshiriki mashindano ya Cecafa U-20 Championship yatakayofanyika nchini Uganda.

Wanasoka hao walifaulu kuchaguliwa kutokana na majaribio yaliyofanyika jana katika uwanja wa Mbaraki Sports Club yaliyoongozwa na kocha wa timu ya taifa ya Harambee Starlets, Charles Okere Okoth.

Okoth alisema zaidi ya wasichana 60 walishiriki kwenye zoezi la majaribio ya jana ambapo 10 watapigania nafasi wakati wa majaribio ya kitaifa hali wengine wawili walichaguliwa kupigania nafasi ya timu kubwa ya Starlets.

Wasichana 10 hao waliochaguliwa kupigania nafasi ya kuwa kikosi cha timu hiyo ya U-20 kutoka Pwani ni Njoki Kamau (Mombasa Olympic), Rael Atieno na Invoilata Mukosh (St John’s Girls).

Wengine ni Mahenzo Katori, Salama Masika, Halima Omar, Mercy Mwalimu, Nelly Kache (wote wa MTG Kilifi), Joy Tsaka (Ocean D) na Catherine Aringo (Fortune Ladies). Wanasoka wawili watakaofanyiwa majaribio na timu kubwa ya Starlets ni Happy Muta (Rabai) na Grace Willy (Ocean D).

Kocha Okoth alisema amefurahikiwa na jinsi wasichana wa Pwani wanavyosakata soka la hali ya juu na wameonelea wafike mashinani kuchaguwa wachezaji ambao wana talanta na wanaoweza kuwakilisha taifa lao kwenye mashindano ya kimataifa.

“Nina imani kubwa tukichagua wanasoka kutoka kila sehemu ya nchi, tutakuwa na kikosi chenye sura ya uzalendo na nashukuru kuwa Nick Mwendwa ana nia kubwa ya kuinua soka ya wanawake kuanzia mashinani,” akasema mkufunzi huyo.

Alisema baada ya kuzunguka sehemu kadhaa za nchi, atachagua kikosi cha wanasoka 30 wanaotarajiwa kupiga kambi kuanzia Agosti 1 kujiandaa kwa mashindano ya Cecafa Challenge Cup U-20 Championship yatakayofanyika kuanzia Agosti 14.

  • Tags

You can share this post!

Red Carpet na South C United zakabana koo, Young City...

Onkar Rai aibuka mwanamichezo bora Kenya mwezi Juni