• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
SGR, barabara nzuri ndiyo rekodi kuu ya Uhuru – Utafiti

SGR, barabara nzuri ndiyo rekodi kuu ya Uhuru – Utafiti

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI ya Jubilee itakumbukwa kwa ujenzi wa barabara na reli ya kisasa (SGR), ripoti ya kura ya maoni inaonyesha.

Utafiti uliofanywa na kampuni ya TIFA unaonyesha kuwa asilimia 47 ya Wakenya wanasema kuwa Rais Uhuru Kenyatta amepiga hatua kubwa katika ujenzi wa miundomsingi nchini tangu alipotwaa hatamu za uongozi mwaka wa 2013.

Rais Kenyatta alikuwa amepanga kujenga kuweka lami yenye urefu wa kilomita 10,000 za barabara kufikia mwishoni mwa muhula wake wa pili 2022.

Waziri wa Uchukuzi, James Macharia anasema kuwa tayari serikali imetia lami kilomita 9,000 za barabara kote nchini na inalenga kupitisha kilomita 10,000 kufikia 2022.

Utafiti huo uliofanywa kati ya Juni 24-28, mwaka huu, asilimia 10 ya Wakenya wanasema kuwa mwafaka wa ushirikiano baina ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga, almaarufu handisheki, umemfanya kiongozi wa nchi kuonekana kama mpenda amani na mpatanishi.

Asilimia nne wanasema kuwa Rais Kenyatta amefana katika usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali. Takwimu za shirika la kusambaza umeme, Kenya Power, zinaonyesha kuwa idadi ya wateja imeongezeka kutoka milioni 2.03 mnamo 2013 hadi milioni 7.57 Julai 2021.

Wengine (asilimia 2) wanasema kuwa wameridhishwa na hatua ya serikali ya Jubilee kutoa fedha kwa wazee, walemavu na watu wengine wasiojiweza pamoja na kupunguza gharama ya elimu.

Lakini asilimia 26 ya watu 1,550 ya walioshiriki katika utafiti huo walisema kuwa hawana habari kuhusu mradi wowote ambao umetekelezwa na serikali ya Jubilee.

Wakati huo huo, ripoti hiyo ya TIFA inaonyesha kuwa asilimia 72 ya Wakenya wanaamini kuwa nchi imepoteza mwelekeo.

Wanaoamini kwamba nchi imepoteza mwelekeo wanasema kuwa gharama ya maisha imepanda, deni la kkitaifa limeongezeka, kuna ukosefu wa ajira, ufisadi umekolea na serikali imeshindwa kudhibiti janga la corona.

Asilimia 12 ya wanaoamini nchi inaendelea vyema, wanasema serikali imefanikiwa kukabiliana na janga la corona, miundomsingi imeimarika, elimu na huduma za afya zimeboreshwa.

Kwa mujibu wa ripoti, wakazi wa eneo la Kaskazini Mashariki ndio wanaoongoza kwa kusema kuwa nchi inaendelea vyema. Wakazi wa Pwani wanaongoza kwa kusema kuwa Kenya imepoteza mwelekeo.

“Changamoto kuu ambazo Wakenya wanasema zinakumba taifa hili ni gharama ya juu ya maisha, ukosefu wa kazi, ufisadi serikalini, umaskini, janga la corona, njaa, ukiukaji wa Katiba, uhasama wa kikabila, deni la kitaifa na kudorora kwa usalama,” inasema ripoti ya TIFA.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Wakenya maskini ndio wameumizwa zaidi na janga la corona baada ya kupoteza kazi na vyanzo vya mapato.

You can share this post!

Kesi za ufisadi: Haji ajitetea

Tumaini shirika la Ubelgiji likifadhili uchimbaji kisima...