• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:06 AM
Zogo lakumba fidia ya wavuvi Lamu

Zogo lakumba fidia ya wavuvi Lamu

Na KALUME KAZUNGU

UTATA umeibuka kuhusu ulipaji fidia kwa wavuvi walioathirika na ujenzi wa Bandari ya Lamu, baada ya kuibuka kuwa orodha ina majina ya watumishi wa umma.

Wavuvi hao wanadai fidia ambayo ingegharimu serikali Sh1.76 bilioni.

Sasa imeibainika kuwa orodha ya wanaostahili kupokea malipo hayo imejumuisha majina ya wafanyakazi wa mashirika makubwa ya serikali, polisi na maafisa wa afya.

Katika mahojiano na wanachama wa kamati hiyo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Makundi ya Wavuvi Lamu (BMU), Bw Mohamed Somo, walikiri kuwepo kwa majina hayo kwenye orodha.

Baadhi ya majina ni ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA), ile ya ukusanyaji ushuru (KRA), kikosi cha polisi miongoni mwa mashirika mengine.

Wanakamati walidai hali hiyo ilitokana na kuwa, baadhi ya watu waliofaa kupokea fidia walifariki ndipo jamaa zao wakajumuishwa kwenye orodha kama warithi.

“Ni kweli utapata majina ya wafanyakazi wa KPA, KRA, madaktari, polisi na hata wanabiashara wakubwa yakiwa kwenye orodha ya wavuvi wanaofaa kufidiwa. Hiyo haimaanishi majina hayo yaliingizwa kwa mlango wa nyuma. Watu wasiwe na shaka. Shughuli tunaifanya kwa utaratibu na uwazi,” akasema Bw Somo.

Maafisa wamedai pia hali hiyo ilitokana na kuwa wamiliki wa mashua za uvuvi huenda ni waajiriwa serikalini, ilhali pia wao waliathiriwa na shughuli za ujenzi wa bandari na ni haki yao kupata fidia.

Fidia hiyo imekuwa suala tatanishi katika Kaunti ya Lamu kwani imecheleweshwa kwa muda mrefu ilhali bandari mpya ya Lamu ilikuwa tayari ishazinduliwa kuanza kutumiwa kwa uchukuzi wa mizigo kimataifa.

Mapema Mei, serikali ilitangaza kuwa ingewafidia wavuvi wote wa Lamu kabla ya mwisho wa mwezi huo lakini hadi sasa ahadi haijatimizwa.

Mwenyekiti wa Muungano wa kutetea haki za jamii wa Save Lamu, Bw Mohamed Athman, ambaye pia ni mwanachama wa hiyo alikiri kuwepo kwa majina ya wafanyakazi wa serikali lakini akatoa sababu sawa na zile za Bw Somo.

Alionya kuwa suala hilo halifai kutumiwa na KPA kuchelewesha kuwapa wavuvi fidia zao.

Hata hivyo, Afisa wa Uhusiano Mwema wa KPA, Bw Bernard Osero alisema kikao kitaandaliwa wiki hii na wadau ili wakubaliane kukamilisha shughuli hiyo nje ya mahakama.

“Tayari zoezi la kukagua akaunti za benki za wavuvi inaendelea. Watu wasiwe na shaka. Watapata fidia yao hivi karibuni,” akasema Bw Osero.

Kamati ya kusimamia ulipaji fidia kwa wavuvi iliundwa mwaka wa 2016 kushirikisha maafisa wa KPA, wavuvi wa Lamu wasimamizi wa mradi wa bandari ya Lamu na shirika la Save Lamu.

You can share this post!

Tumaini shirika la Ubelgiji likifadhili uchimbaji kisima...

Mzozo Tunisia wazidi kutokota Rais akimtimua waziri wa...