• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
EACC yalaumiwa kwa kuhujumu juhudi za kukombolewa kwa fedha za umma Kilifi

EACC yalaumiwa kwa kuhujumu juhudi za kukombolewa kwa fedha za umma Kilifi

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Kilifi Amason Kingi ameilaumu Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa kuwa kizingiti katika juhudi za serikali yake za kukomboa Sh43 milioni zilizoporwa na wafanyakazi wa kaunti hiyo mnamo 2016.

Serikali hiyo ya Kilifi ilipoteza fedha hizo kupitia sakata ambapo wafanyakazi wa idara ya fedha walipitisha fedha hizo kimtandao, kutoka akaunti ya Serikali ya Kaunti ya Kilifi hadi kwa akaunti za kampuni feki.

“Tuliwasilisha kesi kortini na tukafaulu kupewa uamuzi. Lakini kabla ya sisi kupewa kibali cha kukomboa fedha hizo, EACC ilipinga uamuzi huo ikisema kuwa hatukuwa na mamlaka ya kisheria kukomboa fedha zilizoibiwa,” Gavana Kingi akawaambia wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Fedha za Umma (CPAIC) Jumatatu.

Gavana huyo alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Migori Ochilo Ayacko kujibu maswali kuhusu hitilafu za usimamizi wa fedha zilizonakiliwa kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathangu.

Ripoti hiyo ni ya matumizi ya fedha za umma katika kaunti hiyo katika mwaka wa kifedha wa 2018/2019.

Suala hilo la wizi wa mamilioni ya fedha za umma katika kaunti hiyo limekuwa likiibuliwa katika ripoti za afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kila mwaka tangu 2016.

Awali, EACC na kitengo cha kupambana na ulaghai katika benki zilichunguza sakata hiyo na baadhi ya washukiwa wakafikishwa mahakamani.

Ni baada ya hapo ambapo, serikali ya Gavana Kingi iliwasilisha kesi nyingine mahakamani ikitaka kibali cha kuruhusiwa kukomboa fedha hizo kutoka kwa washukiwa wa sakata hiyo.

Maseneta vile vile, walilaumu EACC kwa kuizuia serikali ya kaunti ya Kilifi kukomboa fedha hizo, wakisema hizo ni pesa za umma ambazo zinapaswa kurejeshwa ili zisaidie wakazi wa kaunti hiyo.

“Sh43 milioni ni pesa nyingi mno. Mbona EACC inazuia utekelezaji wa haki? Kama seneti tunapinga hatua hii kwa sababu wajibu wetu ni kutetea masilahi za serikali za kaunti na ufanisi wa ugatuzi kwa ujumla,” akasema Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo.

Mwenyekiti wa CPAIC Bw Ayacko alitoa amri kwamba EACC itoe maelezo ya kina kuhusu suala hilo na kesi ambayo iliwasilisha kuzuia serikali ya Kilifi kukomboa fedha hizo.

“Nimeipa EACC muda wa siku 14 kuwasilisha ripoti hiyo mbele ya kamati kisha tutoe mwelekeo,” akaeleza seneta huyo wa Migori.

Maseneta wanachama wa CPAIC pia walielekeza kidole cha lawama kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwa kutwaa stakabadhi za kaunti ya Kilifi zenye taarifa za matumizi ya fedha na hivyo kuhujumu kazi ya maafisa wa Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bi Gathungu.

“Kutwaliwa kwa baadhi ya faili kuhusu miradi mbalimbali ndiko kulizuia ukaguzi wa miradi tisa ambayo imeorodheshwa kwenye ripoti ya mkaguzi wa hesabu za serikali. Wakati wa ukaguzi, stakabadhi hizo bado zilikuwa zikishikiliwa na maafisa wa DCI,” Bw Kingi akawaambia maseneta hao.

You can share this post!

Pombe haramu lita zaidi ya 300 yaharibiwa katika mitaa...

Mjukuu wa Moi asalimu amri, sasa kupimwa DNA