• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:20 AM
Hofu idadi ya maambukizi ya corona ikipanda tena nchini

Hofu idadi ya maambukizi ya corona ikipanda tena nchini

Na CHARLES WASONGA

KWA mara ya kwanza ndani ya kipindi cha miezi miwili, Kenya mnamo Jumatano iliandikisha zaidi ya visa 1,000 vipya vya maambukizi ya Covid-19 huku serikali ikiwaonya raia dhidi ya kukaidi masharti ya kuzuia msambao wa ugonjwa huo.

Katika takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, jumla ya visa vipya 1,006 vilinakiliwa ndani ya muda wa saa 24 baada ya sampuli 5,584 kupimwa.

Hii inawakilisha kiwango cha maambukizi cha asilimia 18.

Kwenye taarifa iliyotiwa saini na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, kaunti za Nairobi, Kiambu, Kilifi, Mombasa, Nakuru na Uasin Gishu ndizo ziliandikisha idadi kubwa ya maambukizi mapya.

Hata hivyo, kaunti zinazopakana na Ziwa Victoria, ambazo Juni ziliwekewa masharti zaidi ya corona, zilionekana kuandikisha idadi ndogo za maambukizi mapya.

Kulingana na taarifa hiyo, Kaunti ya Nairobi ilinakili maambukizi mapya 391 ikifuatiwa na Kiambu yenye visa vipya 121. Kaunti ya Kajiado (56) , Mombasa (46), Nakuru (42), Uasin Gishu (37), Busia (26), Murang’a (24), Machakos (18).

Kaunti ya Kericho iliandikisha visa vipya 14, Nyandarua (13), Taita Taveta (11), Kirinyaga na Migori visa 10 kila moja, huku kaunti za Bungoma na Nyeri zikiandikisha visa vinane kila moja.

Lamu, Tana River, Nandi na Garissa ziliripoti wagonjwa saba wapya kila moja, na wagonjwa wanne zaidi wakigunduliwa katika kaunti za Baringo na Meru.

Kaunti za Bomet, Kisii, Embu, Kwale na Vihiga ziliandikisha visa vitatu kila moja huku Kakamega na Kisumu zikinakili visa viwili kila moja.

Nazo kaunti za Makueni, Narok, Trans Nzoia, Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet na Isiolo ziliripoti kisa kimoja cha corona kila moja ndani ya saa 24 zilizopita.

Akiongea na wanahabari katika makao makuu ya Wizara ya Afya kabla ya kutolewa kwa takwimu kuhusu hali ya corona nchini, Waziri Kagwe alionya kuwa Kenya ingali hatarini kufuatia ongezeko la visa vya maambukizi mapya vinavyoripotiwa kila siku.

“Tumeshuhudia ongezeko la mahitaji ya vitanda vya ICU na hewa ya oksijeni katika siku za hivi karibuni. Idadi ya wagonjwa wanaohitaji oksijeni ilikuwa imeshuka hadi chini ya watu 100 lakini  Jumanne idadi hiyo ilipanda hadi wagonjwa 400,” akasema.

Bw Kagwe alitoa wito kwa magavana kuhakikisha kuwa hospitali zao zina vifaa tosha vya kupambana na janga la Covid-19 kufuatia ongezeko la idadi ya maambukizi.

“Vile vile, magavana wahakikishe kuwa wagonjwa wanapokea huduma bora kwa sababu taifa lingali linakabiliwa na hatari ya kuathirika zaidi na janga hilo,” akasema

Waziri Kagwe alisema hayo alipoongozwa hafla fupi ya kupokeza kaunti ya Turkana ambulansi zilizotolewa kama msaada kutokana na ushirikiano katika Shirika la Maendeleo Kanda hii, (IGAD) na Umoja wa Ulaya (EU).

Wakati huo huo, wagonjwa 13 waliripotiwa kufariki kutokana na corona, vifo hivyo vyote vikiwa ni vile ambavyo viliripotiwa kuchelewa kutoka hospitali mbalimbali nchini katika mwezi huu wa Julai.

Hii sasa inafikisha 3, 895, idadi jumla ya waliofariki kutoka na Covid-19 tangu mwaka 2020.

Nao jumla ya wagonjwa 261 walithibitishwa kupona ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita; 228 wakiwa ni wale waliokuwa wakitibiwa katika hospitali mbalimbali huku 33 wakiwa ni wale waliokuwa wakiuguzwa nyumbani.

You can share this post!

DPP kumshtaki afisa wa polisi kwa mauaji ya bucha Kiamaiko

Vipusa wa Uingereza kuvaana na Northern Ireland mnamo...